📌FAUSTINE GIMU
WIZARA ya Afya,Maendeleo ya Jamii,jinsia ,Wazee
na Watoto imetoa onyo na kutahadharisha wanaotoa taarifa ama elimu
isiyosahihi na upotoshaji kuhusu magonjwa yasiyoambukiza .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba
10,2021 jijini Dodoma ,Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Aifello Sichalwe amesema
elimu na taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwa njia ya mitandao ,hasa zikilenga
kutoa ushauri wa lishe ,ufanyaji wa mazoezi ,kupunguza uzito ,matibabu ya
magonjwa sugu kama kisukari,saratani na shinikizo la juu la damu.
Mganga mkuu huyo wa serikali amesema kwa
kuwa watoa elimu hawana sifa na weledi hali ambayo hupelekea kuleta
mkanganyiko katika jamii kwa kutoa elimu zisizo sahihi.
Napenda kutoa rai kwa Taasisi ,makampuni na wananchi wenye nia njema ya kusaidia serikali kuelimisha jamii ili kuwezesha kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa ni sahihi kwa kuelimisha jamii kwa kutumia miongozo ya wizara ya afya,kutumia wataalam wenye sifa na weledi katika uelimishaji.
Pia amewataka wadau hao kuwasiliana na wizara kupitia kitengo cha
mawasiliano serikalini kwa ufafanuzi na uratibu wa taarifa mbalimbali.
Aidha,Dkt.Sichalwe amesema wizara ya
Afya,Maendeleo ya jamii,jinsia,Wazee na Watoto inaendelea kuwakumbusha wananchi
wote kuchukua tahadhari zote za kujikinga na magonjwa yasiyo ya
kuambukiza kwa kufanya mazoezi mara kwa mara kulingana na ushauri
wa wataalam,kupunguza matumizi ya chumvi,sukari na mafuta,kuacha matumizi
ya pombe,kuepuka matumizi ya tumbaku na dawa za kulevya.
Pia,katika kuboresha afya na lishe mganga mkuu
huyo wa serikali amewakumbusha wananchi kuzingatia ulaji unaofaa kwa kula mlo
kamili kulingana na mazingira yanayowazunguka huku akitoa wito kwa
wananchi wote kufanya uchunguzi wa awali ili kutambua afya zao na wenye
matatizo kuchukua hatua stahiki za kupata matibabu kwenye vituo vya
kutolea huduma za afya nchini
0 Comments