Waziri wa
Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza baada ya kushuhudia zoezi la utiaji saini
mkataba wa ushirikiano kati ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na
TANESCO kukamilika uliofanyika Dar es Salaam. Aliyeketi chini ni Waziri wa
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile
|
📌PRISCA ULOMI, WMTH
WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetiliana saini leo ya mkataba wa ushirikiano na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ya ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kutumia miundombinu ya umeme ili kuongeza kasi ya ufikishaji wa huduma ya intaneti, simu na televisheni kwa wananchi
Utiaji saini wa mkataba huo umefanywa na Katibu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka kwenye ofisi ya Mkoa wa Ilala, TANESCO, Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani
Dkt. Ndugulile asema kuwa lengo la utiaji saini wa ushirikiano baina ya Wizara yake na TANESCO ni kuhakikisha kuwa Serikali inaongeza maeneo na ushirikiano yatakayopelekea kuongeza tija, kasi ya ufikishaji wa miundombinu ya mawasiliano na usambazaji wa umeme nchini pamoja na kupunguza gharama za ujenzi wa miundombinu hiyo ili palipo na nguzo ya umeme kuwepo na huduma ya intaneti, simu na televisheni kwa kuwa tayari Serikali imefikisha huduma za umeme kwa wananchi mpaka kwenye nyumba za tembe.
Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 170 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 1,880 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo kwa kutumia miundombinu ya umeme ujenzi wa kilomita hizo utaongezeka na kufikia kilomita 4,244 hivyo kuiwezesha Serikali kuwa na jumla ya kilomita 12,563 ifikapo mwaka 2022 kwa kuwa hivi sasa tayari kuna kilomita 8,913 za Mkongo huo
Naye Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa utiaji saini wa mkataba huu leo ni matunda na matokeo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Wizara zizungumze na hii ni dalili njema kwa kuwa wote ni Serikali na tunamhudumia mwananchi huyo huyo na hakuna tofauti baina ya nguzo za umeme na nguzo za mawasiliano za TTCL hivyo kwa wananchi hii tofauti ya miundombinu ya nguzo haipo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akizungumza mbele ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani
Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa mkataba huo utatoa
fursa mpya kwa Wizara kutumia miundombinu ya mawasiliano iliyojengwa na TANESCO
kufikisha huduma za mawasiliano mpaka nyumbani kwa mwananchi; na TANESCO
kutumia miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano itakayojengwa kufikisha
umeme kwa wananchi kwenye makazi yao hivyo kupunguza gharama za ujenzi wa
miundombinu hiyo kwa kutumia mkataba huu na Wizara itashirikiana na TANESCO ili malengo
na maslahi ya Taifa yaliyowekwa yaweze kufikiwa kwa wakati
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameupongeza uongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na TANESCO kwa kusaini mkataba huo kwa kuwa Serikali itakuwa imewasaidia wananchi kupata huduma za mawasiliano na umeme na ametoa rai kwa watendaji wahakikishe utekelezaji wa mkataba huu unafanyika kikamilifu na waendelee kutumia mawazo ya wazee wazalendo wa TANESCO na TTCL kwa kuwa wana utaalam na wanazeeka umri bali mawazo yao bado yako pale pale
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema
kuwa mkataba huo utawezesha matumizi na uwekezaji mpya kwenye miundombinu ya
mawasiliano ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na ya umeme ya TANESCO ambapo
itaongeza kasi ya kuwafikia wananchi kwa kuwa tutakuwa tumefikisha umeme na
mawasiliano kwa mwananchi kwa wakati mmoja hivyo Serikali itakua imeua ndege
wawili kwa wakati mmoja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Dkt. Tito Mwinuka wakibadilisha mkataba wa ushirikiano baina ya Wizara hiyo na TANESCO ya ujenzi wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kutumia miundombinu ya umeme baada ya kusaini, Dar es Salaam. Wanaoshuhudia nyuma ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile, kulia kwake ni Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi akitoa salamu za shukrani baada ya utiaji saini wa mkataba huo amesema kuwa Serikali ni moja na ndiyo inayotoa fedha za kujenga miundombinu hii na inalenga kumhudumia mwananchi huyo huyo hivyo ni jambo jema kwa taasisi za Serikali kushirikiana kwa kuwa mwananchi atapata huduma zote tatu kwa wakati mmoja ikiwemo intaneti, simu na televisheni
Utiaji saini huo umeshuhudiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano
na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati, Henry Mahimbali; Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa; Wakuu wa taasisi
wa TTCL, Shirika la Posta Tanzania; Menejimenti na watendaji wa Wizara mbili
tajwa hapo juu
0 Comments