SAMIA ATOA WITO KWA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUSHIRIKIANA KUJENGA TAIFA.

 

📌AGNESS PETER (DOMECO)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) kuoanisha mipango, vipaumbele na mipango yao na mipango ya kitaifa ili waweze kutekeleza kazi kubwa ambayo wamelenga kuifanya kwa maslahi ya nchi.

Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali(CSO’s) jijini Dodoma, Samia ameyataka mashirika hayo kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa kazi zao na kuandaa mipango yao kwa kuoanisha.

Amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yaliopata usajili ni zaidi ya 11,000 na yanayofanya kazi ni 4663 tu na mashirika kama 7000 aidha hayajulikani yanafanya nini au hayapo,yamekufa au vinginevyo.

‘’Na hii ni kwasababu mashirika mengi yanaanzishwa kwa ajenda iliyopo duniani  kwa wakati ule, ulimwengu ukielekea kwenye mazingira mashirika mengi yatasajiliwa kwenye mazingira ulimwengu ukizungumza watoto na haki zao basi mashirika mengi watoto na haki zao na hii ni kwasababu wanajua 
fedha ipo pahali,nikianzisha taasisi basi fedha itakuja sasa mashirika ya aina hayo ndo yale ambayo hayajulikani yanafanya nini baada ya fedha waliyoilenga kusita,’’ amesema.

Amesema anahimiza mashirika hayo hususani ya ndani kupunguza utegemezi kwasababu ajenda za kidunia zinavyobadilika wahisani na wadau wa maendeleo nao wanabadilisha sera zao na mipango yao ya kutoa fedha.



Amesema wizara kwa kushirikiana na baraza la taasisi zisizo za serikali  wajadiliane na kutengeneza mpango mkakati ambao utasaidia taasisi hizo  kutafuta fedha na kujitegemea.

Rais Samia ameyata mashirika yasiyo ya kiserikali  kufanya kazi zinazoendana na tamaduni, mila, desturi na maadili ya kitanzania na baraza la mashirika hayo kuhimiza washirika wao kuzingatia sheria inayosimamia shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali.

Huko nyuma tulikuwa hatuwezi kuweka mchango wa taasisi zisizo za kiserikali kwasababu ilikuwa kwanza hamkuwa wawazi kwenye kusema mnachokifanya, mnacho kitumia na vipi mnakwenda

Aidha mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Lilian Badi amesema sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini imeendelea kukua na kuimarika kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali hususani afua za afya, ulinzi wa jamii, uwezeshaji wananchi , elimu, kilimo,jinsia, maji, utawala bora na haki za binadamu .



Amesema sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zimechangia kukwamisha ufanisi utekelezaji wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali hapa nchini ikiwa ni pamoja na changamoto ya upatikanaji wa misamaha ya kodi.

Amesema changamoto nyingine ni muda unaotumika kupata vibali vya kutekeleza miradi na afua mbalimbali katika mikoa na mamlaka ya serikali za mitaa na changamoto ya upatikanaji wa vibali vya kazi na ukaazi wa raia wa kigeni wanaofanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiserikali.

‘’Nimatumaini yetu kuwa changamoto hizi zitafanyiwa kazi ili kujenga mazingira rafiki  na wezeshi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuendelea kufanya kazi  kwa ufanisi kwaajili ya maslahi ya wananchi wa Tanzania  na Taifa kwa ujumla,’’ amesema.

 Amesema wanaahidi kuendelea kushirikiana na wizara yenye dhamana kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kupitia ofisi ya msajili  wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kwamba wataendelea kutekeleza shughuli  na majukumu yao kwa kuzingatia  sheria, kanuni na miongozo ya uratibu wa mashirika  yasiyo ya kiserikali  na sheria nyingine za nchi.

 

 

Post a Comment

0 Comments