RAIS SAMIA: SENSA NI MUHIMU KWA UGAWANYAJI NA UTOAJI HUDUMA ZA KIJAMII

 


📌JOSEPHINE MTWEVE, AGNESS PETER NA ZAINAB MTOI (DOMECO)

RAIS wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa zoezi la sensa kwa mafanikio kutasaidia  katika ugawaji wa rasilimali kwa wananchi kama vile elimu, afya, maji, umeme na ujenzi wa miundombinu kwenye maeneo mbalimbali ..

Akizungumza katika uzinduzi wa mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 leo jijini Dodoma, Samia amesema zoezi la sensa linahusisha ukusanyaji wa takwimu ya watu na makazi na taarifa hizo zitawezesha serikali kutoa huduma za kijamii kulingana na idadi ya watu na mahitaji ya maeneo katika maeneo yao.

Ni ukweli kuwa kama huna hesabu au takwimu sahihi huwezi kugawa rasilimali na kutoa huduma kwa haki, uwiano na inavyopaswa kutolewa.

‘’Huwezi kushughulikia changamoto ya ajira endapo huna takwimu sahihi za watu wasio na ajira, huwezi kupeleka huduma zozote kushughulikia matatizo ya watu wenye mahitaji maalumu kama huna idadi ya watu hao,’’ amesema. 

Rais huyo amesema mbali na Serikali, taarifa hizo za sensa hutumiwa pia na jumuiya za kimataifa, sekta binafsi na asasi za kiraia kufanya maamuzi mbalimbali ya kimaendeleo.

Amesema wafanyabiashara na wawekezaji hutumia taarifa hizo za sensa kufanya maamuzi ya aina ya biashara na uwekezaji wawekeze wapi na kwa kiasi gani.

Samia amesema aidha kikanda na kimataifa taarifa za sensa hutumika kupanga, kufuatilia na kupima utekelezaji wa sera, mipango, mikakati na programu mbalimbali za kimaendeleo.

Taarifa za sensa hutumika na watafiti wengi wa ndani na nje ya nchi kama misingi ya kufanyia tafiti nyingine mbalimbali na ndio maana tunasema sensa ni maendeleo tunaomba watu wote wajiandae kuhesabiwa

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali  imepanga kuinua uchumi wa viwanda na kumaliza changamoto ya ajira nchini lakini ili kutimiza malengo hayo ni lazima kuwepo na takwimu sahihi ambazo zinapatikana kwenye taarifa za Sensa.

Mhe Rais naomba nikuhakikishie kuwa kazi hii ambayo umetupatia ya Sensa ya Sita tutaisimamia ipasavyo na kwa weledi wa hali ya juu, nikuhakikishie watu wote watakaolala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa Agosti 2022 wote watahesabiwa

 Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba amesema chimbuko la mkakati huo ni kukabiliana na fikra potofu na mila potofu na kukosekana kwa uzalendo panapokuwepo na masuala ya kitaifa.



Nchemba amesema ipo mifano mingi ambayo pamekuwepo na masuala ya kitaifa na yakakumbana na baadhi ya fikra au mila potofu na kusababisha kupunguza ufanisi wa mazoezi hayo.

‘’Wanatukumbusha wenzetu ambao ni wakubwa kwa umri ,tunaambiwa kwamba hata wakati wa uanzishwaji wa vijiji wa ujamaa ili kuweza kurahisisha kupanga maendeleo na kufikisha huduma za jamii kwa watu wetu tunaambiwa wapo ambao walipinga,’’ amesema.

Amesema hata mkazo ulipokuwa unatolewa kwenye elimu zipo jamii na baadhi ya watu kwenye jamii waliokuwa wanapinga elimu kwa kila mototo wa kitanzania hasa kwa watoto wakike.

Amesema hata kwenye upande wa sensa yamekuwa yakitokea mambo ya fikra potofu, zipo baadhi ya jamii ambazo zimekuwa zikificha watoto walemavu na zingine zikikataa tu watoto wao kuhesabiwa.

‘’Kwahiyo tukaona kabla ya zoezi hili kuanza tupate kipindi cha kutosha cha kuelimishana na tutumie makundi mbalimbali wanayoweza kuongea kwa lugha zao kama wafugaji waongee kifugaji, kama wavuvi waongee kivuvi na kama vijanja waongee kwa lugha zao ili tuelimishane umuhimu wa sensa katika kupanga shughuli za kimaendeleo,’’ amesema Nchemba.

Kwa upande wake mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt.Albina Chuwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu imejipanga kuendesha zaoezi la sense la mwaka 2022 kwa kutumia TEHAMA ili kurahisisha uchakataji wa data.

Dkt.Chuwa amebainisha kuwa mpango mkakati uliozinduliwa hii leo na Rais Samia umelenga katika kuandaa umma katika mambo yote yanayohusu sense hiyo ili kuandaa mazingira bora yakufanikisha zoezi hilo ifikapo mwakani.


Nguli wa Bongo Flavour Ali Kiba akitumbuiza katika tukio la uzinduzi wa Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma


Msanii wa Bongo Flavour Diamond Platnumz akitumbuiza katika tukio la uzinduzi wa Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 lililofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. PICHA NA IKULU.











Post a Comment

0 Comments