RAIS SAMIA AWAAPISHA MAWAZIRI,ATOA NENO WAZIRI MPYA WA ULINZI

 



📌 JOSEPHINE MTWEVE NA ZAINAB MTOI(DOMECO)

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaapisha Mawaziri wapya pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali leo Ikulu  Chamwino, Dodoma.

Akizungumza baada ya uapisho huo Rais Samia amesema lengo la kuwateua mawaziri hao ni kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Rais Samia amebainisha kwamba katika kipindi cha miezi 6 ya Uongozi alitumia muda huo kusoma mienendo ya Wizara na Mawaziri wake,hivyo mabadiliko hayo yana lenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

"Katika miezi 6 ya urais wangu, nilikuwa mkimya na mtulivu nikisoma wizara zinavyoendeshwa. Wakati mimi nawasoma, na wao walinisoma. Kati yao walichukulia ukimya na utulivu wangu kama udhaifu wakaanza kufanya yanayowapendeza. Nilikuwa najifunza, nimeona."- Rais Samia Suluhu Hassan

Hata hivyo amewatahadharisha na kuwataka wateule hao kwenda kuchapa kazi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Mawaziri wapya natumaini mtakwenda kufanya vizuri. Uteuzi wenu hauna maana nyie ni wazuri kuliko waliokuwepo, uzuri wenu utaonekana katika kazi. Hata tuliowateua mwanzo walikuwa wazuri, nataka kuona matokeo sitaki kuwaona kwenye TV tu mnafanya hili na lile

 Rais Samia Suluhu


Rais Samia pia ameweka sababu zilizomshawishi kumteua Dkt.Stergomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi huku akiwatoa shaka Watanzania kuhusu uzoefu wa Waziri huyo mpya wa kwanza Mwanamke kuongoza wizara hiyo.

Amesema uzoefu alioupata Dkt. Tax akiwa katika nafasi mbalimbali katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika( SADC), Dr. Tax na kusimamia vizuri mambo yote ya usalama ndani ya jumuiya hiyo kuna toa matumaini kuwa atasimamia vizuri wizara hiyo.

Nimeamua kuvunja taboo (imani) ya muda mrefu kwamba Wizara ya Ulinzi lazima akae Mwanaume mwenye misuli yake lakini kazi ya Waziri kwenye Wizara ile sio kupiga mizinga wala kubeba bunduki ni kusimamia sera na utawala wa Wizara, nikaamua Dada yetu Dr. Tax nimpeleke huko

 Rais Samia Suluhu

Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango amewataka mawaziri hao wapya kufanya kazi nzuri ili kuleta matokeo kwa wananchi ambao wanatarajia mambo mazuri kutoka kwa serikali yao..

Dkt.Mpango amewaagiza mawaziri hao kwenda kushirikiana na watendaji waliopo kwenye wizara zao ili watimize matarajio ya watanzania na kuwaomba wakasimamie miradi yote mikubwa ambayo serikali inatekeleza kupitia wizara zao.


Makamba ukasimamie sekta kwa uaminifu utupe jicho lako kwa watendaji wa TANESCO, tumuone Mheshimiwa Rais kama kocha, aone wachezaji wake wanavyocheza

Katika uapisho huo, Dk Stergomena Tax ameapishwa kuwa  Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akichukua  nafasi ya  Elias Kwandikwa (marehemu). 

January Makamba ameapishwa kuwa Waziri wa Nishati akichukua nafasi ya  Dk Medard Kalemani ambaye uteuzi wake umetenguliwa na Prof.Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi akichukua nafasi ya Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho ambaye uteuzi wake  nae umetenguliwa.



Dr. Ashatu Kijaji ameapishwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akichukua nafasi ya Ndugulile, Kijaji anachukua nafasi ya Dkt. Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Na Dkt. Eliezer Feleshi amekula kiapo cha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Prof. Adelardus Kilangi aliyekuwa Mwanasheri Mkuu wa Serikali ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.


Post a Comment

0 Comments