📌WFM-DODOMA
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mikopo yenye jumla ya Shilingi bilioni 281.74 kwa ajili ya
kuendeleza miradi ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini kwa wakulima 1,514,695 vikiwemo vyama
vya wakulima 151.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), alipokuwa akijibu swali
la Mbunge wa Tabora Kaskazini Mhe. Athumani Almas Maige, aliyetaka kujua riba za Benki ya Kilimo zinatofauti
gani na riba za benki za biashara ili kumsaidia mkulima mdogo.
“Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeweka
utaratibu wa kutoza riba ya kiwango kisichozidi asilimia 10 kwa kuzingatia
uwezo wa wazalishaji wa madaraja tofauti katika sekta ya kilimo, mifugo na
uvuvi,” alieleza Mhandisi Masauni.
Mhandisi Masauni alisema mikopo inayotolewa kwa wakulima wadogo hutozwa riba nafuu
isiyozidi asilimia 10 na kwa masharti nafuu ya urejeshwaji yanayozingatia
misimu ya mavuno na mauzo ya mazao.
“Sambamba na utoaji wa mikopo ya moja
kwa moja, Benki ya maendeleo ya kilimo inasimamia Mfumo wa Dhamana kwa Wakulima
Wadogo (Smallholder Credit Guarantee Scheme – SCGS) unaolenga kuchagiza mabenki
na taasisi za fedha kuongeza ukopeshaji katika sekta ya kilimo,” alisema
Mhandisi Masauni.
Aliongeza kuwa hadi
kufikia mwisho wa mwezi Juni 2021, Mfumo wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo ilitoa
udhamini wa mikopo kwa wakulima wadogo 11,244, vikundi vya wakulima 181 na SMEs 43 waliopata
mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 89.92 kutoka benki 9 washiriki katika
uendeshaji wa mfuko huo.
0 Comments