📌ASTERIA MUHOZYA NA TITO MSELEM
IMEELEZWA kuwa, pamoja na mambo mengine, ili kufikia lengo la kukusanya Shilingi 650 Bilioni iliyopangiwa Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, Tume ya Madini itaweka nguvu kubwa katika Usimamizi wa Madini ya Viwandani na Ujenzi ili yaweze kuchangia ipasavyo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mtendaji wa Tume ya Madini
Mhandisi Yahya Samamba Agosti 23, 2021 wakati akiwasilisha taarifa ya
Utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Madini na hali ya upatikanaji na Utoaji wa
Huduma katika Masoko kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini
Dodoma.
Aidha, itakumbukwa kuwa, mapema mwezi Mei, 2021 mara tu baada ya Wizara kuwasilisha Bungeni Hotuba yake ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/22, Tume ya Madini iliwasilisha wizarani mapendekezo ya mkakati kuhusu namna ya kufikiwa kwa makusanyo hayo ambapo miongoni mwa yaliyopendekezwa ni pamoja na kuimarishwa kwa usimamizi katika madini ya ujenzi.
Akizungumzia hali ya utoaji na upatikanaji wa huduma katika masoko ya Madini Samamba alisema kuwa, tangu kuanzishwa kwa Masoko ya Madini mwezi Machi 2018, hadi kufikia Juni 2021, jumla ya Masoko ya Madini 41 na Vituo Vidogo vya Ununuzi 59 vimeanzishwa na kuongeza kwamba, kati ya masoko yaliyoanzishwa, 26 ni ya dhahabu, masoko 14 ni ya madini ya vito na soko 1 ni la Madini ya Bati.
Mhe. Mwenyekiti kati ya vituo 59 vya ununuzi wa Madini vilivyoanzishwa, vituo 55 ni vya ununuzi wa Madini ya dhahabu, vituo 2 ni vya ununuzi wa madini ya vito na dhahabu, 1 cha madini ya almasi na 1 cha madini ya vito
Mhandisi Samamba.
Akielezea hali halisi ya mapato katika masoko,
Mhandisi Samamba aliieleza Kamati kuwa, tangu kuanzishwa kwa masoko hayo mwaka
2018 hadi kufikia mwezi Juni 2021, usimamizi wa masoko ya madini umeendelea
kuimarika ambapo katika kipindi rejewa kilogram 32,592.84 za dhahabu, karatu
32,636.59 za Madini ya almasi na kilogramu 144,102.09 za Madini ya bati
ziliuzwa kupitia masoko hayo.
‘’Mchango wa masoko kwenye mapato yatokanayo na Madini umeongezeka kutoka asilimia 2.62 mwaka 2018/19 hadi kufikia asilimia 26.44 mwaka 2020/21,’’ aliongeza Mhandisi Samamba.
Akizungumzia mchango wa masoko ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2020.2021, alisema masoko hayo yamechangia kiasi cha shilingi bilioni 145.23 sawa na asilimia 26.44 ya mapato yatokanayo na mrabaha na ada za ukaguzi ikilinganishwa na mwaka 2019/20 ambapo masoko hayo yalichangia kiasi cha shilingi bilioni 104.63 sawa na asilimia 21.28.
Aidha, akielezea matazamio katika Masoko ya Madini aliyataja
baadhi kuwa ni pamoja na mapato yanayotokana na madini yanatazamiwa kuongezeka
kutokana na kufutwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa Madini
yanayoingizwa ndani ya nchi, kurejea kwa mnada wa Madini ya vito Arusha ambako
kunatarajia kuvutia uingizaji wa Madini ya vito na ununuzi kutoka nchi za nje
na hivyo kuchochea mzunguko na mitaji ya wafanyabiashara wakubwa kuongezeka.
0 Comments