WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi
wa Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma.
“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu, amedhamiria
kuendeleza miradi yote ikiwemo ya ujenzi wa makao makuu na miradi mbalimbali
inayofanyika hapa Dodoma. Hatua hii ni uthibitisho tosha kwa Watanzania kuwa
kazi zinaendelea.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Agosti
13, 2021) baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Ikulu mpya Chamwino,
Dodoma ambao umefikia asilimia 78.
Ujenzi wa Makao Makuu bado unaendelea, Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza kazi zote ziendelee zikiwemo za ujenzi wa Mji wa Serikali hapa Dodoma.
Amesema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi bilioni
131 zitatumika katika ujenzi wa majengo ya magorofa ya makao makuu ya wizara
kwenye Mji wa Serikali, Mtumba.
Aidha, Waziri Mkuu amesema shilingi bilioni 169
zitapelekwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya maboresho ya jiji
hilo ikiwemo miundombinu ya barabara, maji na umeme.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akutane na Mawaziri wenzake ili waanze mchakato wa ujenzi majengo ya wizara.
Ujenzi huo unatakiwa uanze Septemba, mwaka huu na ufanywe na kampuni za ukandarasi za Serikali pamoja na kampuni za sekta binafsi
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Ikulu
ya Chamwino, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa mradi
huo na hatua iliyofikiwa na kwamba ana imani utakamilika kwa wakati.
“Leo nimefarijika kuona maendeleo ya ujenzi wa
mradi huu na furaha hii inatokana na hatua tuliyoanzia na tulipofikia sasa.
Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitaka kuona Ikulu mpya
inafanana na ya Dar es Salaam na leo nimeona kweli zinafanana.”
0 Comments