WIZARA ya Kilimo kwa
kushirikiana na wadau inaendesha makongamano kuhusu mifumo ya chakula kwa lengo
la kukusanya maoni yatakayosaidia nchi
kuboresha mifumo ya chakula na
kuimarisha lishe ikiwa ni utekelezaji wa malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya
Umoja wa Mataifa (SDGs).
Akifungua kongamano la
mifumo ya chakula kwa wakulima,
wafugaji, wavuvi na wadau wengine wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini leo
(01.07.2021) mjini Njombe kwa niaba ya
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Mkurugenzi Msaidizi Sera na
Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mbaraka Stambuli, alisema mikoa ya Njombe
,Songwe, Ruvuma na Rukwa inaongoza kwa kuwa na watoto wenye udumavu .
Aliongeza kusema mikoa
ya Nyanda za Juu Kusini ndio inaongoza kwa kwa uzalishaji mkubwa wa chakula
lakini jambo la kushangaza ukanda huu ndio wenye hali duni ya za lishe.
Stambuli alisema
kongamano la mifumo ya chakula linalenga kujadili changamoto muhimu katika
mifumo ya chakula kwa kuzingatia ikolojia kwenye kanda ili kufanya dunia kuwa
na uhakika wa chakula na lishe bora.
Kwa mfano mkoa wa Njombe ndiyo wenye asilimia kubwa ya Watoto wenye udumavu (53.6%) amba[o mikoa mingine yenye udumavu zaidi ya asilimia 40 ni Songwe (43.3%), Ruvuma (41.0%), Rukwa ( 47.9 %) na Iringa (47.1%) ambapo takwimu hizi zinaashiria matatizo katika mfumo wa chakula hivyo wadau wanatakiwa kutafuta majawabu kuboresha hali ua lishe nchini
Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu Mifugo alibainisha kuwa mfumo wa chakula una mafungamano na changamoto ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi pia mwenendo mbaya wa hali ya hewa, magonjwa sugu, maonjwa yasiyo ya kuambukiza na lishe duni ikiwemo athari za kutozingatiwa u salama na ustawi wa wanyama.
Stambuli alibainisha
kuwa Wizara ya Kilimo imepewa jukumu la kuratibu na kuhakikisha wadau wote wa
sekta ya umma na binafsi katika mfumo wa chakula wanashiriki mijadala ambapo
mapendekezo ya nchi yatawalishwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa
utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu New York Marekani.
Akizungumza kuhusu
lengo la kongamano la mfumo ya chakula Mwakilishi toka Wizara ya Kilimo Magret
Natai alisema maana ya ‘ Mfumo wa Chakula ni mkusanyiko wa shughuli
zinazohusiana na uzalishaji ,usindikaji,usafirishaji ,uhifadhi na ulaji wa
chakula ‘.
Natai alibainisha kuwa
kupitia kongamno hilo wadau watapata muda wa kujadiliana mifumo sahihi
itakayoongeza kasi ya namna dunia inavyozalisha, inavyotumia chakula na mtazamo
wake kuhusu chakula.
Wakizungumza kwenye
kikao hicho wawalikishi wa wakulima kutoka Njombe,Iringa,Mbeya ,Songwe na
Ruvuma wakiwemo Benno Mgaya kutoka
SAGCOT Songea alisema ili kukabiliana na changamoto za udumavu elimu kwa shule
za msingi na sekondari ni muhimu ikiwemo suala la lishe bora.
“Ni muhimu shule zote nchini ziwe na bustani za mboga mboga na matunda ili kuwajengea watoto uelewa wa umuhimu wa lishe bora wakiwa bado wadogo” alisisitiNaye Martin Haule mfugaji kutoka wilaya ya Njombe alisema Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alisisitiza suala la lishe bora ili kuepukana na hali ya udumavu ambapo amewataka wazazi kutoa chakula bora na kwa wakati kwa watoto wao .
Haule alibainisha kuwa
kwa Njombe tatizo la udumavu linachangiwa na “ wazazi kwenda mashambani na
kurudi jioni hivyo watoto wanashinda na njaa au watoto wanapewa ulanzi na
komoni badala ya chakula bora hivyo udumavu kuendelea” alisema.
Majadiliano kuhusu
mifumo ya chakula yanafanyika nchini kwenye kanda mbalimbali chini ya uratibu
wa Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula Dkt. Honest Kessy (Country Converner) aliyeteuliwa kuratibu
mijadala hii kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Andrew Massawe.
Kongamano la Mifumo ya
Chakula Nyanda za Juu Kusini Njombe linafanyika sambamba na jingine
linalofanyika Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza ili kupata mapendekezo ya nchi na
hatua za kuimarisha mifumo ya chakula yakihusisha wadau wa maendeleo wakiwemo
AGRA, FAO, WFP, GAIN na SAGCOT.
Imeandaliwa na :
Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Kilimo
NJOMBE
01.07.2021
0 Comments