📌DOTTO KWILASA
SERIKALI imewaita kazini
watumishi wa kada ya afya waliopo chini ya Wizara ya Afya wapatao 473 kujaza
nafasi zilizoachwa wazi kutokana na watumishi mbalimbali kufariki,kukoma
utumishi na kustaafu.
Hatua hiyo imekuja kufuatia
Wizara hiyo kutoa kibali Cha ajira mbadala za kada mbalimbali za Afya Kupitia
tovuti ya Wizara mnamo Mei 12 Mwaka huu zilizotokana na watumishi kukoma
utumishi kutokana na sababu mbalimbali.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Profesa Abel Makubi wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusiana na ajira hizo huku akisisitiza kuwa watu hao
wameitwa kutokana na kukidhi vigezo vya ajira.
Watumishi waliochaguliwa watakuja kujaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi mbalimbali ambao walistaafu,waliofariki na wengine kuacha kazi.
Prof.Abel Makubi
Hata hivyo amefafanua kuwa
kutokana na nafasi hizo 473 zilizotangazwa na Wizara hiyo,walipokea jumla ya
maombi 19757 ambapo kati ya hayo maombi 4760 yalikosa sifa kutokana na
kutokamilisha taratibu za uombaji.
"Wengi hawakukamilisha
taratibu za uombaji kwa kushindwa kuambatanisha vyeti vya taaluma huku Baadhi
wakiomba nafasi ambayo sio taaluma yao hivyo maombi yao kutokidhi
vigezo,hivyo basi maombi 9338 ndiyo yamekidhi vigezo na sifa za
kuajiriwa,"amefafanua.
Sambamba na hayo Prof.Makubi
ameeleza vigezo vilivyotumika kuwapata waombaji hao Kuwa ni Pamoja na
kuzingatia waombaji wenye ulemavu,wenye ajira za mikataba ya muda,waombaji
wenye umri chini ya miaka 45 na waombaji waliohitimu elimu ya Mwaka 2018 na
kurudi nyuma.
Kwa umuhimu huo amefafanua pia
mgawanyo wa nafasi hizo 473 kwa kada mbalimbali kulingana na walivyopokea
kutoka Ofisi-Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora kwamba katika kada ya
Daktari bingwa idadi ya nafasi zilizohitaji kibali ni Saba na waliochaguliwa ni
Saba.
Daktari daraja la pili 23,Daktari wa meno 5,Afisa Muuguzi 17,Afisa Muuguzi msaidizi 67,nafasi ya Muuguzi 140,Afisa afya mazingira 3 na Afisa afya mazingira msaidizi 3.
Licha ya hayo amezitaja nafasi
nyingine za Fundi sanifu vifaa tiba nafasi 1 , Fiziotherapia nafasi 2,Katibu wa
afya 1,Famasia 7,Mteknolojia-Meno 3,Mteknolojia-Mionzi 5,Mteknolojia Maabala 10
,Myeknolojia-Macho 5, Mteknolojia Msaidizi Maabala 8 Pamoja na Msaidizi wa afya
166.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu
huyo amewataka waliochaguliwa katika nafasi hizo kuripoti katika Hospitali ya
Mirembe Jijini Dodoma kuanzia leo hadi Julai 9 Mwaka huu wakiwa na nakala
halisi pamoja na vivuli vya vyeti.
0 Comments