📌PRISCA ULOMI
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.
Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali itahakikisha mawasiliano ya utangazaji
yanafika kote nchini kwa kuwa mawasiliano ya redio yanawapata taarifa mbali mbali
wananchi na Wizara tunapenda kuona maudhui ambayo yanaendana na utamaduni wetu
Tanzania na yanajibu changamoto za wananchi kwa kuwa sasa kuna taarifa ambazo
sio sahihi zinatolewa kwa wananchi kupitia baadhi ya vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii.
Ameongeza kuwa Serikali itapunguza gharama za leseni
za redio jamii na za pembezoni zilizopo ngazi ya Wilaya ili kuondoa adha ya
wananchi waishio pembezoni mwa mipaka ya nchi yetu kwa kusikiliza redio za nchi
nyingine za jirani
Dkt.
Ndugulile ameyasema hayo leo akiwa Mgeni Rasmi
kwenye uzinduzi na makabidhiano ya studio ya kisasa ya kidijitali ya TBC ya redio
jamii ya Mjini Dodoma kwa kuwa ukarabati, ununuzi na ufungaji wa mitambo ya studio
hiyo umegharamiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambayo ni moja ya taasisi
zilizo chini ya Wizara hii. Aidha, ameahidi kuwa Wizara itaangalia namna ya
kushirikiana na Shirika la utangazaji Tanzania (TBC) kuwezesha upatikanaji wa njia
maalumu na kifaa cha satelaiti cha kutunza na kuhifadhi taarifa za studio hiyo
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni
na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameishukuru Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari kuwezesha ukarabati na kufunga mitambo mipya ya studio ya redio jamii
ya TBC iliyopo Dodoma ambayo itasikika kwenye mkoa wa Dodoma, Singida, Iringa
na maeneo ya jirani kwa kuwa moja ya kipaumbele cha Wizara ya Habari ni
kuiwezesha TBC kifedha, mtaji na kuendeleza wataalam.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kuwa Kamati
imeridhishwa na studio hii mpya ya TBC kwa kuwa Bunge limekuwa na nia hii na
leo limetimia ili wananchi wapate taarifa za Serikali kwa kuwa vyombo vya habari
vipo vingi ila TBC ni chombo cha uhakika na wananchi wanapenda kusikiliza
taarifa kutoka TBC
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka amesema kuwa
redio ya jamii ni nzuri ili wananchi wa eneo husika wapate taarifa zinazowahusu
na watahakikisha taasisi za Serikali za Mkoa wa Dodoma zitatumia studio hii
kutangaza taarifa zao kwa wananchi mathalani masuala ya maji, umeme na kulipia
matangazo ili studio iweze kujiendesha
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema kuwa
taasisi yake imetoa shilingi bilioni 1.07 kukarabati, kununua na kufunga
mitambo ya studio hiyo ambapo mwakilishi wa Bodi ya UCSAF, Mhandisi Francis
Mihayo ameiomba bodi ya TBC kuhakikisha mitambo iliyonunuliwa inatunzwa na
kutumika kuendana na thamani ya fedha iliyonunulia
Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba amesema kuwa
TBC wametoa shilingi milioni 163 kukarabati studio hiyo na imeunganishwa na
redio nyingine ya TBC Taifa na TBC FM na kufafanua kuwa huu ni mwanzo wa
kuendeleza Dodoma kimawasiliano kwa kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na
Serikali.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
0 Comments