CELINA
MWAKABWALE(UCSAF)
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe,
Dkt. Faustine Ndugulile amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa
Wote(UCSAF) imetangaza zabuni mbili za miradi ya kufikisha huduma za
mawasiliano katika maeneo ya mipakani na kanda maalum awamu wa sita. Zabuni
ambayo ina kata 190 zenye vijiji 380 na imetengewa kiasi cha shilingi za
kitanzania 26,830,000,000.
Zabuni ya pili ni ya mradi unaolenga kufikisha
huduma za mawasiliano katika ofisi za Halmashauri na kanda maalum na umetengewa
ruzuku ya fedha za kitanzania 10,880,000,000 ukiwa na kata 34 zenye vijiji 45.
Waziri Ndugulile amesema hayo katika hafla ya
uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Wizara wa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha
2021/22 hadi 2025/26 uliofanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wakiwemo Manaibu Waziri, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso, wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara na mjumbe
kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar.
Mradi wa kufikisha huduma za mawasiliano mipakani unalenga
kuhakikisha kuwa maeneo yote ya mipakani yanapata mawasiliano ya uhakika ili
kulinda na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi huku mradi wa kufikisha huduma
za mawasiliano katika ofisi za Halmashauri na kanda maalumu unalenga kuboresha
huduma za mawasiliano katika maeneo hayo.
Akizungumzia Mpango Mkakati wa wizara, Dkt. Ndugulile
amesema umejikita katika nyaraka mbalimbali za kisera, malengo ya maendeleo ya
kitaifa na kimataifa pamoja na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2021-2025
katika vipengele vinavyogusa mawasiliano na teknolojia ya habari.
Awali akifanya wasilisho kwenye banda la UCSAF mbele
ya Waziri Ndugulile na viongozi wengine wa Serikali waliombatana nae, Mtendaji
Mkuu wa UCSAF Justina Mashiba amesema katika kipindi cha siku 200 tangu kuundwa
kwa Wizara hiyo, Mfuko umefanikiwa kukamilisha miradi ya mawasiliano ya simu
katika kata 84 zenye vijiji 305 na wakazi zaidi ya laki saba wamenufaika na
mradi huo.
Aidha ameongeza
kuwa, Mfuko umekamilisha mradi wa kuboresha usikivu wa radio katika eneo la
Mradi wa kimkakati wa Bwawa la Umeme pamoja na maeneo ya Kisaki, na kwa kushirikiana
na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Zanzibar, Mfuko umefanikiwa
kuanzisha kituo cha Mawasiliano ya dharura (Emergency call centre) kwa lengo la
kuratibu taarifa za matukio ya dharura yanayohitaji uratibu wa pamoja kama
kutoa taarifa za matukio ya moto, mafuriko na maambukizi ya magonjwa kama vile
ugonjwa wa COVID-19.
0 Comments