NAIBU Waziri wa
Kilimo Hussein Bashe amesema wizara imefanikiwa kutekeleza agizo la Rais Samia
Suluhu Hassan kuhusu utambuzi wa wakulima ambapo hadi sasa kupitia Mfumo wa
M-Kilimo tayari wakulima 1,979,662 na Maafisa Ugani 6,840 wamesajiliwa kwenye
mfumo hatua inayosaidia kufikisha huduma za ugani na masoko kwa haraka.
Bashe ametoa kauli hiyo leo (04.07.2021) wakati
alipoongea na Waandishi wa habari ofisini kwake Dodoma ambapo amesema lengo la
wizara ya kilimo ni kusajili wakulima takribani milioni 6 kupitia kaya zao
hatua itakayosaidia utambuzi na ufikwishwaji wa huduma za ugani ili kuwezesha
tija kwenye kilimo kupatikana.
Aliongeza kusema kuwa ili wizara iweze kuwahudumia
wakulima ni lazima kuwatambua na kufahamu mahala walipo ndio maana ikaanzisha
mfumo wa kiteknolojia wa usajili wa wakulima (M-Kilimo) ambao sasa umefika
mikoa yote ya Tanzania Bara.
" Katika bajeti ya mwaka 2021/22 wizara imepanga
kufundisha maafisa ugani (re-training) ili waweze kusaidia wakulima kuongeza
tija kwenye uzalishaji mazao ambapo ili lengo hilo lifanikiwe lazima uwatambue
wakulima ndio maana tumeanzisha mfumo huu wa Mobile Kilimo ambapo wakulima
wanasajiliwa kupitia maafisa ugani kwenye kata." aliema Bashe.
Akizunguza juu ya umuhimu wa mfumo huo Naibu Waziri Bashe
alisema mfumo M-Kilimo utasaidia kupima kazi zaMaafisa ugani Kilimo katika
maeneo ya kiutendaji kwa kuwa takwimu zinaonesha kila ushauri alioutoa kwa
mkulima ikiwa ni wa ana kwa ana (physical consultation) au kupitia njia ya
mtandao (online consultation).
“ Hadi sasa jumla ya maswali ya wakulima yapatayo 7,792
yamepokelewa na kujibiwa na maafisa Ugani Kilimo kupitia mfumo wa M-Kilimo
unaoratibiwa na Wizara ya Kilimo” alisisitiza Bashe na kuongeza kuwa wizara
inatarajia kufungua kituo cha huduma kwa wakulima (Call Centre) kuwezesha
wakulima kupiga simu na kujibiwa maswali yao kwa haraka zaidi.
Katika hatua nyingine Bashe ametaja mikoa iliyofanya
vizuri kwenye usajili wa wakulima kuwa ni Morogoro (153,977), Njombe (153,158)
na Mara (148,772) huku mikoa ambayo bado ipo chini ikiwa ni Pwani imesajili
wakulima 14,784) na Mtwara (28,000) .
Kufuatia hatua hiyo Bashe ametoa wito kwa wakurugenzi wa
halmashauri nchini kuwawezesha maafisa ugani wao wa wilaya kusajili na
kuhamasisha wakulima ili waingie kwenye mfumo wa M-Kilimo kuwezesha kufikia
lengo la kukuza tija kwenye uzalishaji mazao ya kilimo kupitia huduma bora za
ugani.
Ili kuleta ufanisi kwenye usajili wa wakulima Naibu
Waziri huyo wa wizara ya Kilimo alisema kupitia bajeti 2021/22 inatarajia
kununua simu za mkononi za kisasa (smartphones ) na kuzigawa kwa Maafisa Ugani
kote nchini ili zitumike kusajili wakulima
kwa kutumia teknolojia maalum (App)
Naye Mratibu wa Mfumo wa M-Kilimo Rajab Mkalange amesema
mfumo huu ni wa kiteknolojia unaoweza kumsaidia mkulima kupata huduma za ugani
na masoko kupitia maswali kwenye simu yake ya kiganjani kuwasiliana na Afisa
Ugani ngazi za kijiji, kata, wilaya na Wizarani.
Aliongeza kusema mfumo huu tangu uliopanza kufanya kazi mwanzoni
mwa mwaka huu umewezesha kupunguza tatizo la upungufu wa maafisa ugani kwa kuwa
wakulima wanaweza kupata huduma hizo pale wanapokuwa wamesajiliwa kwenye mfumo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mifumo ESRF John Kajiba alisema
taasisi yake ilifanya utafiti kwenye mikoa ya Kagera na Mara kuhusu mahitaji ya
wakulima kwenye huduma za ugani na kugundua kuwa wakulima wanahitaji taarifa za
huduma za ugani na masoko kwa haraka kutaboresha tija kwenye Kilimo.
Kajiba aliongeza kusema kuwa kupitia utafiti huo ndipo wakaanzisha
ushirikiano na Wizara ya Kilimo kuanzisha mfumo wa M-Kilimo unaotekelezwa kote
nchini .
Wakulima wanaweza kujiunga na Mfumo wa M-Kilimo kupitia
simu zao za mkononi ambapo wanaweza kubonyeza *152*00# na kuchagua neon Huduma
za Serikali kisha kubofya namba 7 Kilimo.
Imeandaliwa na :
Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
DODOMA
04 Julai, 2021
0 Comments