📌DOTTO KWILASA
SERIKALI imeazimia kuendeleza utekelezaji
wa mkakati wa kutokomeza ukatili na mauaji ya wazee nchini ili kukuza ustawi
haki na ujumuishi wazee na hatimaye waishi maisha yenye afya, hadhi na salama.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mwanaid Ali
Khamis amesema hayo jana jijini Dodoma wakati wa
maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wazee.
Amesema kuwa katika kutimiza azma ya kuendelea kuwalinda
wazee pamoja na kuimarisha huduma nyingine, serikali ipo katika hatua za
mapitio ya sera ya Taifa ya wazee ya 2003, ambayo inaweka msisitizo katika
kuimarisha upatikanaji wa haki ya ulinzi na usalama kwa wazee.
Aidha, amesema kuwa sera inayofanyiwa mapitio inalenga
kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi katika jamii ya kuwalinda wazee kutokana
na hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili, pamoja na mifumo ya upelelezi na
uendeshaji wa mashauri ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wazee.
Kutokana na ukweli kwamba hali duni ya kipato ni miongoni mwa sababu zinazochangia vitendo vya ukatili kwa wazee, serikali inalenga kuhakikisha wazee wanawezeshwa katika kubuni na kuendesha shughuli za ujasiriamali kupitia vikundi vidogo vidogo katika jamii ili kuwawezesha kuinua kipato na kumudu mahitaji yao ya msingi
Pia, amesema kuwa wazee watawezeshwa
kushiriki katika shughuli za michezo na burudani ili kuimarisha afya zao
na kuwajenga kisaikolojia.
Amesema, katika jitihada hizo za kuimarisha ulinzi kwa
wazee, serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea na mapambano ya kutokomeza
vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee kwa kuongeza msukumo na kuimarisha
uratibu wa utekelezaji wa Mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee kwa
kipindi cha miaka mitano (2018/2019-2022/2023).
Hata hivyo, amesema kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa
na serikali kwa kushirikiana na wadau, vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee
nchini vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
“Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi, mauaji ya
wazee yamepungua kwa kiwango kikubwa kutoka 577 mwaka 2014 hadi wazee 34
Desemba 2020”alisema
Vilevile, alisema kuwa serikali inadhamiria kuongeza
jitihada na kuhakikisha mauaji ya wazee yanakwisha kabisa.
“Serikali katika mapitio ya sera ya wazee ya mwaka 2003
imezingatia kuweka msisitizo zaidi katika kuhakikisha wazee wanapata huduma ya
msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha ili kusaidia kuimarisha afya na ustawi
wao”alisema
Amesema kuwa kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa wa Utoaji wa
Huduma za Msaada wa Kisaikolojia wa Mwaka 2021, matatizo mengi ya kiafya na
kimahusiano yanayowakabili wazee yanatibika kikamilifu kupitia msaada wa
kisaikolojia na ushauri nasaha.
Kadhalika amesema kuwa kupitia Mpango wa
serikali wa kuboresha huduma za afya, imeendelea kuhakikisha kuwa kila
kituo cha afya cha na hospitali zinakuwa na madirisha
maalum kwa ajili ya matibabu kwa wazee.
“Mpaka sasa kuna jumla ya madirisha 2,335
mahususi kwa ajili ya kutolea huduma za matibabu kwa wazee”alisema
Meneja Program, haki na ushirikiano wa wadau kutoka shirika
la Help Age Intrnational Tanzania, Joseph Mbasha alisema kuwa shirika hilo ni
miongoni mwa mashirika mtandao yaliyopigania utambulisho huo na lina dira ya
kuona dunia ambayo kila mzee anaishi maisha yenye afya, hadhi na usalama.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo shirika hilo linatekeleza
afua tano, ambazo ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya zilizo rafiki na
bora kwa wazee.
Alisema afua nyingine ni kupinga vitendo vya ukatili na
manyanyaso dhidi ya wazee, kutoa huduma jumuishi wakati wa majanga, kuhakikisha
usalama wa kipato, pamoja na kuchagiza harakati za mabadiliko.
Kutokana na hayo ,Tume ya haki za binadamu na Utawala
bora(THBUB)imesema kuwa kunahitajika kuwekwa kwa mifumo madhubuti ya kulinda na
kutetea haki za makundi maalum yanayohitaji ulinzi wa jamii husika.
Akitoa salamu za Tume hiyo , Kamishna wa THBUB,
Dkt. Fatma Khalfani kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji Mstaafu,
Mathew Mwaimu, katika Maadhimisho hayo alisema kuwa Katika kutekeleza
suala hili nchini,Ibaraya12(2)na Ibaraya14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano waTanzania
ya mwaka1977 pamoja na marekebisho yake,zimeeleza juu ya wazee kupewa
heshima na kupata hifadhi kutoka kwa jamii wanamoishi.
Dkt.Khalfani aliongeza kuwa heshima kwa wazee kwenye jamii
zetu nyingi za kiafrika na Tanzania imekuwa ikipewa kipaumbele na mara zote
wazee wamekuwa sehemu ya familia.
Kutokana na umuhimu huo alisema,Tume inawasihi wadau wote kuenzi
na kudumisha utamaduni huo kwa kutekeleza wajibu wao,ikiwemo kuwapatia wazee
ulinzi na usalama,chakula,malazi na mavazi.
"Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka
2002,Tanzania ilikuwa na wazee 1,952,041(sawa na wanaume 940,229 na wanawake 1,011,812)na
katika sensa ya mwaka 2012 idadi ya wazee ili ongezeka hadi kufikia
2,507,568(wanaume1,200,210 na wanawake1,307,358) sawana5.6%ya wananchi
wote,"alisema.
0 Comments