📌JASMINE SHAMWEPU.
UHARIBIFU wa mazingira unasababisha athari kubwa katika uso wa dunia na kukwamisha maendeleo ya watu kwa ujumla. Mwandishi wetu katika makala haya anabainisha changamoto za athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu na kuangalia kwa kina jitihada za Serikali na wadau wake kukabili hali hiyo.
Wataalamu wanajaribu kuweka mpangilio wa changamoto kuu za uhifadhi wa mazingira katika maeneo matatu na kuzibainisha kama matishio ya usalama wa ardhi, misitu, bahari na maziwa, misitu na milima au kwa ujumla usalama wa dunia na maisha ya watu.
“Changamoto Kuu ni upotevu wa bayoanuai unaosababishwa na utawala hafifu na dhaifu wa rasilimali, uvunaji wa rasilimali uliopitiliza na zaidi ni ushiriki dhaifu wa wadau katika uhifadhi wa mazingira na raslimali zilizomo kama wanyama, ndege, samaki, wadudu, misitu na viumbe hai wengine,” anabainisha Nuhu Salasala, Afisa Uraghabishi wa Sera kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Hifadhi ya Wanyamapori, WWF Tanzania.
Nuhu Salasala anafafanua kuwa makosa mengine yanatokana na kuongezeka kwa masoko ya rasilimali hizo na baya zaidi ni uelewa mfinyu wa masuala ya rasilimali hizi kwa kuzingatia thamani ya bioanuai na sera zake.
Katika jitihada za kujaribu kuhifadhi mazingira kwa kushirikisha wadau, taasisi ya kimataifa ya Mfuko wa Maendeleo wa kuhifadhi wanyamapori (World Wildlife Fund) imeanzisha mradi wa Kupaza Sauti za Bioanui – Huu ni mradi wa kulinda uasili na watu unatekelezwa katika nchi 6 ikiwemo Tanzania ambayo kwa upande wake umeanzia Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikisha wananchi.
Mradi umeundwa katika namna yakuzisaidia nchi hizo 6 kutatua changamoto zao za Biashara Haramu za Wanyamapori (Illegal Wildlife Trade) na usimamizi wa mifumo ya kiekolojia kwa njia ya Usimamizi Shirikishi (Inclusive Conservation) na Uchochezi wa Majawabu ya Kiasili (Nature Based Solution).
Akiwasilisha mada kwenye warsha ya mafunzo ya Sera, uraghabishi, uhifadhi shirikishi na masuluhisho ya kiasili chini ya mradi wa kupaza sauti za bioanuai iliyofanyika mwishoni mwa wiki Nuhu Salasala anabainisha maeneo mengine matatu muhimu yanayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huu kuwa ni pamoja na biashara haramu ya maliasili, jitihada za kufanya usuluhisho kwa njia za kiasili na uhifadhi shirikishi unaotumia mbinu za uhifadhi jumuishi.
Changamoto ya kutengwa kwa jamii katika ushiriki wa kuhifadhi mazingira kunapunguza uwiano wa kinguvu ambao unapunguza uwezo wa wazawa na wanajamii kujihusisha na kuchangamana na Watunga Sera na Wafanya Maamuzi, katika mambo ya msingi (Critical issues) kama kupambana na biashara haramu ya wanyamapori duniani ambayo kwa mwaka inathamani ya dola bilioni 23 na ya uvunaji haramu wa magogo kwa mwaka dola bilioni 13.
Wazawa wengi wapo mstari wa mbele katika viti hizi, hivyo kuwasaidia kwa kuwashirikisha, kusikiliza sauti zao, na kuwafanya wawajibike ni wa muhimu sana
Kutokana na changamoto hizi kutishia usalama wa dunia ipo mikutano iliyofanyika duniani kuweka mikakati ya kutokomeza ujangili wa aina zoye na kuhimiza ushiriki wa wadau wa aina mbalimbali. Kwa mfano Mkutano maarufu wa Brazili ulioitwa Rio Summit wa mwaka 1992 - ulizitaka nchi wanachama kutambua na kusaidia utambulisho wa wanajamii, tamaduni na vipaumbele vyao na kufanikisha ushirikishwaji wao ili kufikia Maendeleo Endelevu.
Wadau wakiwa kwenye ufunguzi wa Mradi wa kupaza Sauti mkoani Morogoro |
Aidha ripoti za IPBES (2019) na WWF (2018, 2020), zinahimiza na kuonyesha kwa vitendo uongozi na usimamizi wa pamoja na kwamba kutengwa huku kunapunguza uwiano wa kinguvu ambao upunguza uwezo wa wazawa na wanajamii kujihusisha na kuchangamana na Watunga Sera na Wafanya Maamuzi, katika mambo ya msingi (Critical issues) kama kupambana na biashara haramu ya wanyamapori duniani ambayo kwa mwaka inathamani ya dola bilioni 23 na ya uvunaji haramu wa magogo kwa mwaka dola bilioni 13.
Shirika la WWF lilianzishwa mwaka 1961, ambapo kwa mujibu wa tovuti yake hivi sasa linaendesha miradi zaidi ya 1300 duniani kote na Tanzania ikiwa na miradi kadhaa iliyoendeshwa kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikisha shule za msingi na sekondari, mabaraza ya wazee katika vijiji, uongozi wa kata na halmashauri, mashirika yasiyo ya kiserikali, wafanya biashara na Serikali katika ngazi za mikoa.
Baadhi ya miradi yake ni pamoja na kilimo cha mwani ndani ya maji. Wajasiriamali wengi hutumia rangi zitokanazo na zao hili kutengeneza nguo za batiki na matumizi mengine ya rangi mbalimbali. “Hili ni zao rafiki kwa binadamu na mazingira ya maji ambapo wakulima wanajipatia fedha nyingi huku wakishiriki hifadhi ya mazingira,” anasema Nuhu Salasala.
Mradi mwingine ni kilimo cha mikoko ambayo imebainishwa kuwa na uwezo wa kunyonya hewa ya ukaa mara nne zaidi kuliko mazao mengine. Anafafanua faida ya kunyonya hewa ya ukaa kwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kwa watu wanaokata miti, kuchoma misitu na kusababisha mosho unaopaa angani na kukutana na hewa ya ukaa, husababisha utando na kuongeza joto la dunia ambalo ni9 hatari kwa usalama wa viumbe hai, kwani madhara yake ni kusababisha mvua nyingi zinazoleta mafuriko au kiangazi kinachonyausha mazao na kusababisha upungufu wa chakula duniani.
“Mifano ipo mingi
lakini kwa uchache tunaangalia kuyeyuka kwa theluji juu ya Mlima Kilimanjaro,
kushindwa utabiri wa hali ya hewa kwa kubadilikabadilika kwa mfumo wa mvua,
kupanda kwa bei ya mafuta ya kula kutoka shilingi 12,000 hadi 15,000 na kuruka
hivi sasa kufikia shilingi 35,000 kwa lita tano za mafuta ya alizeti. Hii ni
kwa sababu mvua hazikutosheleza mahitaji ya zai la alizeti katika msimu
uliopita,” anafafanua Nuhu Salasala.
Mbali na miradi hiyo WWF iliendesha mradi ya kudhibiti uvuvi haramu kwa kutumia mabomu aina ya dynamite yanayolipuliwa na waxuxi haramu na kusababisha madhara makubwa ikiwemo kuteketeza mazalia ya samaki hasa kwenye ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi kutoka Tanga hadi Mtwara.
Mradi huu umefanyika kwa ufanisi mkubwa kwa ushirikiano na Serikali kwa kutoa elimu kwa wavuvi na jamii zinazoishi kando ya Bahari hiyo ambayo ilipata uelewa na kushiriki kimailifu kudhibiti uvuvi haramu hata kwa kutoa taarifa zilizosaidia kuwakamata wavuvi haramu na kuwachukulia hatua za kisheria
anaongeza Nuhu Salasala na kusisitiza kuwa suala hilo kwa sasa limepungua au kutokomezwa kabisa.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais Dk Philip Mpango alimtaka Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Seleman Jafo kusimamia utekelezaji wa kampeni kabambe ya kitaifa ya usafi na usimamizi wa mazingira nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Sanjari na hilo alisema Serikali itakuwa inawachukulia hatua kali za kisheria wahalifu wote wa mazingira kwani vitendo vya uharibifu wa mazingira ni dhuluma na ukatili kwa vizazi vijavyo hivyo haviwezi kuvumilika duniani kote.
Dk Mpango alitoa wito huo mwanzoni mwa mwezi huu Jijini Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya mazingira Duniani iliyoambatana na uzinduzi wa kampeni kabambe ya Kitaifa ya usafi na usimamizi wa mazingira nchini.
Katika hatua nyingine ameagiza wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) na halmashuri zote nchini kuongeza jitihada za kusimamia misitu na mapori ya hifadhi yaliyo chini yao na rasilimali zake ikiwa pamoja na kuzuia moto, kukusanya tozo ipasavyo na kupanga matumizi ya rasilimali za misitu ili iweze kuwanufaisha Watanzania wa leo na vizazi vijavyo huku akisisitiza matumizi ya nishati mbadala na kuhimiza wadau wa maendeleo kutekeleza makubaliano ya kimataifa juu ya kulinda mazingira na kudhibiti kuenea kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumzia kampeni hiyo kabambe ya Kitaifa ya usafi na usimamizi wa mzingira nchini, ambayo kauli mbiu yake ni mazingira yangu, Tanzania yangu, naipenda daima huku akiwaelekeza watendaji wa wizara, wakuu wa mikoa, mamlaka mbambali za serikali za mitaa na wadau wengine kuhamasisha wananchi katika utunzaji wa mazingira, kukabiliana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, na kufuatilia utekelezaji kwa karibu na kutolea taarifa
Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Seleman Jafo alitoa wito wa kujenga uzalendo katika utunzaji wa mazingira.
Naye Mwenyekiti wa
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda biashara na Mazingira David Kihenzile,
alisema kazi ya Bunge ni kushauri na kuisimamia Serikali huku akitaka Serikali
kuja na sera bora ambayo itasaidia kutokomeza matumizi ya mkaa.
bado kuna changamoto ya uchafuzi wa mazingira hasa katika uvunaji na matumizi ya kuni na mkaa, hivyo ni vyema Serikali ikatizama kwa kina matumizi hayo ya nishati kuu inayotumika kwa wingi hapa nchini na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Kwa upande wao baadhi ya wadau wa kuhifadhi mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu akiwemo Clara Makenya ambaye ni mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa na muamko mkubwa katika suala la utunzaji wa mazingira. Clara Makenya amesisitiza uhusiano wa shirika hili na Serikali na kuahidi kuendelea kuwa bega kwa bega na tayari kushirikiana kwa kuendeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya uhifadhi wa mazingira.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mazingira kitaifa mwaka huu ni tutumie nishati mbadala, kuongoa mifumo ya ikolojia.
Wakati huohuo Serikali
imezindua Mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya tabia nchi wa
Mwaka 2021-2026 huku ikiitaka jamii kuishi kwa kufuata misingi ya ajenda za
kimazingira kwa kuzingatia makubaliano ya Paris ambayo tayari yamefanyiwa
maandalizi ya rasimu na mchanganuo wa Kitaifa na malengo ya maendeleo endelevu
(SDGs).
“Mkakati huo utasaidia kuondokana na uharibifu wa mazingira uliopo,” amesisitiza Jafo wakati wa uzinduzi wa mkakati huo Jijini Dodoma, hafla iliyokwenda sanjari na Kongamano la Mazingira ambalo limeshirikisha Wadau mbalimbali wa Mazingira kutoka ndani na nje ya nchi yakiwemo mashirika ya UNDP na Care International.
Waziri Jaffo alisema
kuwa inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 1.6 wa ukanda wa pwani
watakabiliwa na changamoto za mazingira ifikapo mwaka 2030 ikiwa jamii
haitaacha shughuli za kibinadamu zinazoathiri mazingira.
Awali Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mary Maganga alisema
Kongamano hilo lilitafakari mada mbalimbali ikiwemo ya matumizi ya
nishati mbadala ili kuongoa mifumo ya ikolojia na kupunguza hewa ya ukaa na
hivyo kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
0 Comments