MWANDISHI WETU, WINDHOEK, NAMIBIA.
TANZANIA imeendelea kung'ara ndani ya Bara la Afrika kwa kutangaza vyema
vivutio vyake vya Utalii ambapo imeweza kuwa miongoni mwa nchi 10 bora
kwa mwaka wa tatu mfululizo, kuanzia 2017 hadi 2020.
Ripoti hiyo imetolewa mapema leo kwenye mkutano wa Kimataifa wa Utalii wa
Kanda ya Afrika ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la Utalii
Duniani (UNWTO), Mtaalamu wa utangazaji wa Utalii, Bi. Olga Nowak
aliitangaza Tanzania kushika nafasi ya saba ambayo inakuwa ni mara ya
tatu.
Katika mkutano huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akiwa
ameambatana na Watalaamu wake kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii
wanashiriki ambapo Waziri Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania imejaliwa kuwa
na vivutio vingi na vya kipekee ambavyo havipatikani mahali popote duniani
isipokuwa Tanzania
Katika kumi bora hiyo, Afrika ya Kusini imetajwa kushika nafasi ya kwanza ikifutiwa na nchi ya Misri katika utangazaji vyema ya vivutio vyake vya utalii.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akifanya kikao cha ana kwa ana mbobezi wa kimataifa wa kutangza vivutio vya Utalii kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa la Utalii ( UNWTO) Bi. Olgo Nowak mara baada ya kufanya wasilisho lake lengo la kuzijengea uwezo nchi za Afrika kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Afrika kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha katika ripoti hiyo, Tanzania imetajwa kuendelea kuongoza na kufanya
vizuri katika sekta ya utalii licha ya uwepo wa changamoto wa ugonjwa wa
UVIKO19 ambao umeikumba karibu Mataifa mbalimbali duniani kote.
Tanzania imekuwa na vivutio mbalimbali vinavyotamba Duniani ikiwemo mlima mrefu
barani Afrika, Mlima Kilimanjaro, Hifadhi zenye vivutio vikubwa vya Wanyama
kama Hifadhi ya Serengeti, Hifadhi ya Nyerere, Hifadhi ya Ruaha, Tarangile,l
pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro
Pia, Tanzania imepata fursa ya kutoa maoni yake kwa lengo la kuimarisha utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo Bara la Afrika ikizingatiwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vivutio vingi na vya kipekee katika Bara la Afrika ambapo Waziri Dkt. Ndumbaro amemkaribisha Mtaalamu wa masuala ya utangazaji kuja Tanzania kutoa ujuzi huo.
0 Comments