📌MWANDISHI WETU
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
imeitaka Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama iendelee kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ili kubaini vitendo vya
unyanyasaji dhidi ya Watu Wenye Ulbino.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar Es Salaam na
Mwenyekiti wa time hiyo Jaji Mstaafu Mathew P.M. Mwaimu katima Maadhimisho ya
siku ya kimataifa ya kuongeza uelewa kuhusu ualbino inayoenda sambamba na
kuhamasisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya watu wenye ualbino, ikiwemo
kuwatambua na kutatua changamoto zinazowakabili.
Mwenyekiti huyo alisema ikiwa Serikali itatumia
nguvu juhudi kuwashughulikia
wanaowanyanyasa na kuwateka albino,wananchi Wataachana na imani, mila,
desturi na mitazamo potofu ambavyo huwafanya Watu Wenye Ualbino kunyanyaswa,
kujiona hawakubaliki, hawawezi na hawana mchango kwa jamii inayowazunguka na
Taifa kwa ujumla katika shughuli zinazohusu maendeleo.
"Wadau
wote Waungane pamoja kutoa elimu kwa
jamii na kupinga vitendo vyote vya udhalilishaji, unyanyasaji na mauaji ya Watu
Wenye Ulbino, hususan wanawake na watoto,"alisema..
Licha ya hayo alisema tume inatambua jitihada
mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kutatua changamoto za watu wenye
ualbino japo jitihada zaidi zinahitajika ili kuondoa kabisa changamoto za watu
wenye ualbino na waweze kufurahia haki zao kama zilivyo katika Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984, na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 ambazo zinasisitiza utu wa
mtu kuheshimiwa.
Ualbino ni hali inayosababishwa na ukosefu wa rangi ya asili (melanin) mwilini ambayo huonekana kwenye rangi ya ngozi, macho na nywele, yaani kama mtu mwenye ualbino ni mwafrika, basi anakosa rangi ya asili ya waafrika wenzake,Ualbino uko katika jamii zote duniani
Alieleza Kuwa Maadhimisho ya mwaka huu ni ya sita
(6) kimataifa, na ya 17 kitaifa, ikiwa na maana kuwa Tanzania ilianza kufanya
maadhimisho ya aina hii hata kabla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuyazindua
rasmi mwaka 2015.
"Kauli mbiu ya maadhimisho haya kimataifa ni: Imara zaidi licha ya changamoto zote ikiangazia ustahimilivu na mafanikio ya watu wenye ualbino wanaokabiliwa na imani potofu, ukatili na ubaguzi kote duniani,Kitaifa maadhimisho haya yanafanyika Jijini Dares Salaam na yanabeba kauli mbiu isemayo: “Vunja Ukimya, Komesha Unyanyasaji kwa Wanawake na Watoto wenye Ualbino”alifafanua Mwaimu.
Vilevile alifafanua kuwa Kauli mbiu hiyo inaangazia
changamoto kuu dhidi ya watu wenye ualbino, ya ubaguzi, unyanyapaa, ukatili na
mauaji kutokana na imani potofu na uelewa mdogo kuhusu ualbino katika jamii.
"Kutokana na hali hiyo Taifa na Dunia nzima
imeshuhudia vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watu wenye ualbino, hususan
wanawake na watoto, vitendo ambavyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu,ni dhahiri
kuwa hali hiyo inaashiria hitaji la kutolewa kwa elimu zaidi kwa jamii kupitia
njia mbalimbali kuhusu ualbino na haki za binadamu,"alisisitiza.
Siku hii Pamoja na mambo mengine ilipitishwa na
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa Azimio Na. A/HRC/RES/23/13 Disemba 18, 2014,
na ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2015. Tangu wakati huo, kila ifikapo tarehe
13 Juni dunia imekuwa ikiadhimisha siku hii ya Kuongeza Uelewa Kuhusu Ualbino.
0 Comments