SERIKALI YAANZISHA SEKTA MAHSUSI YA UJENZI KUBORESHA MIUNDOMBINU

 


📌DOTTO KWILASA. 

ILI kuboresha sekta ya Mawasiliano nchini, Serikali imeanzisha sekta mahsusi ya ujenzi  kusimamia miundombinu ya barabara, vivuko, nyumba, majengo yanayomilikiwa na Serikali pamoja na viwanja vya ndege.


Mbali na majukumu hayo, pia ni kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na sekta hiyo zinaendana na mikakati ya Serikali ya kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu anayesimamia Sekta hiyo, Mhandisi Joseph Malongo, alikukutana na watendaji wa taasisi zilizo chini ya sekta hiyo kwa dhumuni la kuwakumbusha na kuwapa mwelekeo wa Serikali na matarajio ya wadau katika miradi inayotekelezwa.

Katika kufanikisha hilo, Mhandisi Joseph Malongo, alianza kwa kuhakikisha taasisi zote zenye malalamiko ya utoaji wa huduma kutoka kwa wadau anakutana nazo na kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto hizo ili kuboresha utendaji na huduma kwa wateja wa taasisi hizo.


Hivyo, alikutana na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakati wa kuzindua vitendea kazi vya karakana na viti vya wenye uhitaji maalum vitakavyotumika kwenye vivuko vyote nchini.



AFANYA UTAFITI KAZI



Mhandisi Malongo alieleza kuwa alifanya utafiti kuhusiana na utendaji wa TEMESA kutoka kwa wadau mbalimbali.


Katibu Mkuu Malongo alieleza kuwa TEMESA imebweteka kwa sababu imepewa mamlaka kisheria na Serikali kuwa ni taasisi pekee ya Serikali inayotengeneza magari na mitambo.



Mbali na hilo, alieleza kuwa amegundua wafanyakazi wa TEMESA hawaendani na mabadiliko ya teknolojia hususani katika masuala ya magari na mitambo, kwani magari yanayonununuliwa na Serikali kwa sasa ni ya kisasa zaidi ambayo yanahitaji utaalamu wa kipekee.


Alieleza kuwa pia alibaini uwepo wa ukiritimba unaofanywa na baadhi ya watumishi wa TEMESA ambao si waaminifu kwani huduma zinacheleweshwa bila sababu za msingi hata kwa matatizo yanayoweza kutatuliwa kwa muda mfupi.



Mhandisi Malongo alieleza kuwa wadau walimweleza kuwa baadhi ya vipuri vinavyofungwa kwenye magari siyo halisi, hivyo kuharibika muda mfupi baada ya gari kutoka karakana za TEMESA.


Mbali na hilo, Mhandisi Malongo alieleza kuwa wadau walilalamikia kuhusu huduma mbovu zinazotolewa na TEMESA ikiwemo Karakana kutokuwa na sehemu ya mapumziko na sehemu ya kuosha magari baada ya kupatiwa huduma.



“Nilivyoingia wizarani mwezi Aprili mwaka huu niliamua kufanya utafiti kwa baadhi ya taasisi za serikali kuhusu utendaji wa TEMESA, nilifanya hivyo kwa sababu nilikuwa mlalamikaji kuhusu huduma zinazotolewa na TEMESA, matokeo niliyopata kutokana na utafiti wangu ni kuwa asilimia 75 ya niliowahoji walisema kuwa TEMESA wamebweteka, pia wafanyakazi wao kutokuendana na mabadiliko ya teknolojia,” Alisema Mhandisi Malongo.

ATOA MAAGIZO


Kutokana na malalamiko hayo, Mhandisi Malongo aliwataka TEMESA kubadilika na kuwaagiza kuanzisha mkakati madhubuti ambao utaboresha huduma zao, kuongeza ufanisi kwa watumishi ili kuvutia wateja ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu utoaji wa huduma.


Pia, aliwataka TEMESA kuhakikisha unaboresha mkakati wake wa kibiashara, kuboresha usimamizi wa kifedha ambao utalenga kutoa huduma nzuri kwa wateja wao.


Vilevile, aliagiza TEMESA kudhibiti gharama kubwa za matengenezo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa, hivyo alipendekeza kuwa makubaliano maalumu kati  ya Wakala huu na Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) na Toyota Limited yafanyike haraka badala ya kubaki kwenye maandishi.


Mhandisi Malongo pia aliaigiza TEMESA kuwajengea uwezo wahandisi 92 waliopo ili wawe wabobezi katika fani zao mbalimbali, wapatiwe motisha ambayo itaongeza chachu ya kujituma kwa ufanisi.



Mbali na kutoa maagizo hayo, Mhandisi Malongo, aliupongeza uongozi wa TEMESA kwa jitihada ya kukusanya madeni wanayowadai wateja yenye thamani ya Shilingi bilioni 27 kutoka Sh. bilioni 38.


Pia, aliwakumbusha kuwa wateja kutokulipa siyo sababu kwamba hawana fedha bali hawaridhiki na huduma wanayopata kutoka TEMESA.



Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, aliomba kurudishwa kwa mfuko wa matengenezo ya magari kwa ajili ya kupunguza madeni jambo ambalo lilipingwa na Katibu Mkuu Mhandisi Malongo na kusema kuwa kutawafanya TEMESA kuendelea kubweteka na kutotoa huduma bora kwa wateja.


MAFANIKIO/UFANISI WA TEMESA


Mhandisi Maselle, alisema kuwa katika kuboresha huduma za karakana TEMESA imeendelea kukarabati karakana za mikoa ya Dar es Salaam zilizopo eneo la Vingunguti, pamaoja na mikoa ya Mwanza na Mbeya.


Kuhusu ununuzi wa karakana sita zinazohamishika pamoja na vifaa 30 vya kuchunguza ubovu na hitilafu za magari na mitambo, Mhandisi Maselle alisema kuwa vifaa hivyo vitasambazwa katika mikoa ya kikanda ambayo ni Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, Tabora na Dodoma.


Maselle alifafanua kuwa lengo la ununuzi wa karakana zinazohamishika ni kwa ajili ya kusogeza huduma kwa wateja walio mbali na karakana za mikoa, pia kutoa huduma ya matengenezo ya dharura yanayotokea maeneo yasiyo na karakana hasa magari na mitambo yanapokuwa safarini au nje ya ofisi.


Aliongeza kuwa viti vya wenye mahitaji maalum vitakuwa msaada kwa abiria wenye mahitaji maalum, kwamba awali huduma hiyo ilikuwa haitolewi kwenye vivuko vya Serikali na kusababisha usumbufu kwa abiria wenye mahitaji hayo.


Baadhi ya wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi),Mhandisi Joseph Malongo (hayupo pichani), wakati wa uzinduzi wa vitendea kazi vilivyonunuliwa na Wakala huo, Jijini Dodoma.



Kuhusu vifaa vya kuchunguza ubovu wa hitilafu za magari na mitambo, Mhandisi Maselle, alisema kuwa TEMESA imepanga kupeleka vifaa hivyo katika kila kituo na kufafanua kuwa vifaa hivyo vitasaidia kubaini tatizo kwa usahihi na kwa muda mfupi.

Alisema pia kutaboresha huduma na kupunguza muda wa matengenezo ya magari na mitambo pamoja na malalamiko ya wateja kufungiwa vipuri visivyo halisi.

Mwenyekiti wa Bodi ya TEMESA, Profesa Idrissa Mshoro, aliiomba Serikali kupitia wakala huo kuendelea kuajiri mafundi wa kutosha, ili kuongeza idadi ya mafundi na kuwapatia ujuzi utakaoendana na mabadiliko ya teknolojia ambayo itawasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi.


Zaidi ya Sh. milioni 765 zimetumika katika ununuzi wa vitendea kazi vya TEMESA, ambapo kati ya hizo Sh. milioni 494 zilitumika kununua karakana  sita zinazohamishika, Sh. milioni 257 zilitumika kununua vifaa 30 vya kuchunguza ubovu na hitilafu za magari na mitambo na Sh. milioni 13 zilitumika katika ununuzi wa viti 33 vya wenye uhitaji maalum.

TEMESA imeanzishwa kwa Sheria ya Wakala Na. 30 yamwaka 1997 na marekebisho yake ya mwaka 2009, ikipewa majukumu ya msingi ikiwa ni pamoja na kufanya matenegenezo ya pikipiki, magari na mitambo ya Serikali pamoja na watu binafsi.
Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments