LEAD FOUNDATION YAZIFIKIA KAYA 200,000 MRADI WA UTUNZAJI MAZINGIRA

 


📌ZENA MOHAMED

ILI kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi mazingira nchini,Shirika lisilo la kiserikali  la LEAD FOUNDATION linalojihusisha na mradi wa kisiki  hai,limeanzisha Miradi mitatu ya kuhifadhi mazingira katika Mkoa wa Dodoma.

Hatua hiyo imekuja kufuatia ripoti ya hali ya  Mazingira  nchini kuonyesha kiwango cha ukataji wa miti katika Mkoa wa Dodoma kufikia wastani wa hekta 3730,000 kwa mwaka na kusababisha hali ya ukame na uhaba wa maji.

Hayo yamesemwa jijini hapa Leo  na Mratibu wa Programu wa Shirika hilo Mshana Elieneza wakati akiongea na waandishi wa habari katika maonyesho ya wiki ya mazingira ambapo alisema maendeleo ya jamii yoyote hutegemea mazingira bora.

Ametaja  miradi hiyo kuwa ni kukijanisha Mkoa wa Dodoma,kukijanisha Tarafa ya Mima na Kibakwe na Ufugaji nyuki safu za milima Kiboriani ili kurejesha uoto wa asili .

Amesema,  kutokana na uharibifu  mkubwa wa mazingira wao kama Shirika  wameweza kutoa elimu kwa wakulima zaidi ya 2300 katika vijiji 400,kaya zaidi ya 200,000 katika wilaya zote za Dodoma.

Mbali na hayo ameeleza kuwa,katika utekelezaji wa miradi hiyo  kwa kipindi cha miaka mitatu wamepanda miti zaidi ya milioni 5 hali aliyoeleza kuwa imerejesha malisho ya mifugo na miti mingi mashambani ambayo inapunguza joto ardhini na kuleta mvua.

‘‘Katika  kukabiliana na hali ya uharibifu wa mazingira nchini, Lead Foundation hatutaishia hapo tu tumeazimia kustawisha jumla ya miti milioni 14 katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma lengo ni kuokoa hekta laki mbili kwa kustawisha miti ya kisiki hai milioni mbili kwa kila wilaya za mkoa wa Dodoma"Amefafanua

Akiongea zaidi amesema ili kuweza kurudisha uoto wa asili na kupambana   na uharibifu wa mazingira uliokithiri  mkoani hapa kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha anajitoa kwa hali na Mali katika uendelevu wa uoto wa asili.

Sisi kaa wadau wa mazingira hatupendi kuona tunabaki nyuma ,lazima tuwe mstari wa mbele kuhamasisha jamii kwa wilaya zote mkoani hapa kuyajali mazingira

 Elieneza amesema katika Msimu  wa Kilimo ni vyema wakulima  kuacha visiki hai katika  mashamba yao ili kuleta manufaa katika familia zao kwakuwa itasaidia kubadilisha mazingira na kuleta mvua za kutosha pamoja na kuni pia.

Post a Comment

0 Comments