DKT GWAJIMA AUNDA KAMATI,AIPA SIKU 30

 


📌DOTTO KWILASA

WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameunda Kamati ya Mpito yenye wajumbe 10 wa mashirika yasiyo ya kiserikali na kuipa siku 30 ili kuhakikisha wanasimamia uchaguzi wa viongozi na wajumbe wa Baraza la Taifa la mashirika hayo kutokana na uongozi uliopo kushindwa kutekeleza maagizo iliyopewa kwa mara tatu mafululizo. 

Dk.Gwajima alisema hayo  jana Jijini hapa  kwenye kikao chake na Vyombo vya habari huku akiitaka kufanikisha malengo mahsusi. 

Hatua hiyo imekuja kufuatia Desemba 3 mwaka 2019,Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (1) (j) na (m) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002, kuliagiza Baraza kufanya uchaguzi wa viongozi wa Baraza hilo kwa kuwapa muda wa miezi nane (08) kuanzia tarehe 31.3.2020 mpaka tarehe 30.11.2020 kutokufanyika. 

Hata hivyo, Waziri huyo alisema Baraza hilo lilishindwa kutekeleza maagizo hayo kwa kipindi walichopewa na Bodi hiyo iliwaongezea tena kipindi cha siku 14 kuanzia tarehe 3.3.2021 mpaka tarehe 17.3.2021, ambapo pia walishindwa kutekeleza maagizo hayo hivyo, Bodi kupitia kikao chake cha 46 kilichofanyika tarehe 22.4.2021, ilitoa siku 40 hadi kufikia tarehe 1 Juni 2021 Baraza liwe limefanya uchaguzi.

"Mpaka kufikia tarehe 1.6.2021, Baraza lilishindwa kutekeleza malekezo hayo Kwa hiyo, kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 38 (1) na (2) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002, kuhusu usimamizi wa Sheria hii na utekelezwaji wa kanuni zake, ikiwemo Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2016, naagiza uchaguzi huo ufanyike haraka ili kuwezesha vyombo vya usimamizi wa Mashirika hayo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria,"alisema.

Pamoja na hayo alieleza kuwa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyoya Kiserikali (NaCoNGO) limeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 25 (1) cha Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 na kwamba  kwa mujibu wa Kifungu cha 25 (2) cha Sheria hiyo, Baraza ni mwamvuli kwa Mashirika yote yaliyosajiliwa Tanzania Bara.

"Kwa mujibu wa Kanuni 5 (a) (iv), 5 (b) (ii) na 5 (c) (v) ya Kanuni za Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2016, Baraza linatakiwa kufanya Uchaguzi wa Viongozi na wajumbe wa Baraza kila baada ya miaka mitatu (03),

Waziri Gwajima alisema Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mara ya mwisho lilifanya Uchaguzi wake mwaka 2016, ambapo kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi, viongozi hao muda wao wa kukaa madarakani uliisha mwaka 2019. 

Pia aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Flaviana Charles  Mwenyekiti wa Shirika Mtandao la Coalition for Women Human Rights Defenders in Tanzania (CWHRDsTZ),Francis Kiwanga Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS),Dkt. Tulli Tuhuma – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la JSI Research and Training Institute (JSI) na Edward Porokwa – Mratibu wa Shirika Mtandao la Pastoralist Indigineous Non-Governmental Organizations Forum (PINGOs Forum).

Wajumbe wengine ni Pamoja na Tike Mwambipile – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA),Yassin Ally – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini Womens Rights Organization (KIVULINI),Anna Kulaya – Mratibu wa Kitafa wa Shirika la Women in Law and Development Africa (WiLDAF) na Audax Rukonge – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agicultural Non State Actors Forum (ANSAF).

 

"Gunendu Roy – Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la BRAC Maendeleo Tanzania (BRAC) pamoja na Dkt. Astronaut Bagile – Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Women in Social Enterpreneurship (WISE),"alifafanua Dkt.Gwajima.

 

Post a Comment

0 Comments