WIZARA YA KILIMO YAJIDHATITI KUPAMBANA NA SUMUKUVU,YAANZA NA ELIMU KWA WAANDISHI WA HABARI

 


📌RHODA SIMBA

WIZARA ya Kilimo  imesema imejidhatiti kuweka mikakati ya  kukabiliana na sumukuvu kwa kuanza ujenzi wa miundo mbinu sahihi ya kuhifadhia mazao na   kutoa elimu kwa wakulima  na wasindikaji  namna bora ya kukabiliana nayo.

Hayo yamesemwa  leo jijini hapa na  Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama wa chakula Josephine Amollo (pichani juu) wakati akifungua semina  ya waandishi wa habari 100 kutoka mikoa 9  hapa nchini juu ya uchafuzi wa sumukuvu na athari zake katika usalama wa chakula afya na uchumi.

Amesema tatizo la sumukuvu sio Tanzania tu bali in tatizo la nchi nyingi na mara nyingi husababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi lakini serikali imejipanga kuhakikisha kuwa kinachozalishwa kinakuwa salama

Nchi yetu iko salama na chakula kipo salama hakuna tatizo kama ilivyokuwa mwaka 2016 baada ya watu kudhurika na masuala ya sumukuvu.

" Lengo la kuwapa elimu hii waandishi wa habari tunataka wakawe walimu wakaielimishe jamii na kuondoa taharuki ambayo inaleta sintofahamu kwa jamii tunaamini wanahabari hawa watafikisha elimu sahihi kupitia vyombo vyao vya habari,"alieleza.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mazao ambayo yanaathirika zaidi na sumukuvu ni mahindi na Karanga na kuitaka jamii kufuata utaratibu sahihi kuanzia wakati wa kupanda hadi kuhifahi mazao yao.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Kilimo Revocatus Kasimba amesema toka mradi huu wa kudhibiti sumukuvu kuanzishwa kumesaidia kupunguza kuenea kwa janga hili na kupelekea wakulima kuzalisha mazao yenye tija. 

Amesema ili kudhibiti kuendelea kutokea kwa sumukuvu ni vyema mikakati madhubuti ikawekwa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima na watumiaji wa mazao ya chakula kama Karanga na Mahindi.

Naomba waandishi wa habari mtumie vizuri semina hii ya siku mbili (2) kwa sababu jamii inawategemea, ukitumia hata kipande cha sekunde 10 kutoa elimu kuhusu sumukuvu utakuwa umeokoa kizazi cha sasa na badaye 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma(CPC) Mussa Yusuph ameipongeza Wizara ya Kilimo  kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo  kwa Waandishi wa habari kwani wengi wamekuwa wakiripoti matukio yanayohusu sumukuvu lakini hakuna uelewa wa kina kuhusu tatizo hilo.



Amesema mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa kwa waandishi na kutoa taarifa ambazo zimekamilika na hatimae kupitia wao jamii itaelimika na kubadilika.

"Mafunzo haya yatazaa matunda kwa jamii kupitia kalamu za waandishi wa habari.Waandishi tuwe watulivu tusikilize kwa makini ili kila aliyeshiriki mafunzo haya asitoke bure bali akapate elimu ambayo itasaidia na watu wengine,"amesema



Sehemu ya Waandishi wakilisikiliza moja ya wasilisho kuhusu sumukuvu.


 

Post a Comment

0 Comments