📌NTEGHENJWA HOSSEAH(TAMISEMI)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu amesema Wauguzi ni miongoni mwa wataalamu
wa Afya wanaopaswa kuheshimiwa na kupewa thamani inayostahili na wasichukuliwe
kisiasa.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati alipokuwa
akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani yakiyofanyika Mkoani
Manyara tarehe 12 Mei,2021.
Amesema
uuguzi ni fani adhimu na kuwataka viongozi wa Mikoa na Wilaya kuacha
kuwadhalilisha kwa kuwaweka ndani kwa tuhuma zisizo na ushahidi.
“Viongozi wa Mikoa na Wilaya niwatake kuelewa kuwa
uuguzi ni taalamu adhimu na muache kuamuru wawekwe ndani au kuwachukulia hatua
kali ambazo haziendani na taalum yao kwa tuhuma ambazo hazina ushahidi, hili
tuliache mara moja,”amesema
Ameongeza "Kama Muuguzi amekosea akashitakiwe
kwenye Baraza la Wauguzi na Wakunga ambapo atachukuliwa hatua kwa matakwa ya
taaluma yake na sio kwa utashi wa kisiasa.”
Hata hivyo, amesema kiongozi yeyote atakayemuweka
ndani muuguzi awe amethibitisha ameiba
lakini kwa tuhuma nyingine akashitakiwe
kwenye Baraza lao la Kitaaluma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu akikagua maonyesho ya Wauguzi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi iliyofanyika Mkoani Manyara
Pia Mhe.Ummy amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri
kuacha kuwakatalia wauguzi kwenda kusoma mara wanapopata fursa za kwenda
kujiendeleza kielimu.
"Wauguzi lazima wathaminiwe kwa kazi kubwa
wanayoifanya ya kuhudumia wagonjwa sababu mara zote ukienda hospitali Daktari
atakuona kwa muda mchache sana na wakati mwingi utakuwa na nesi katika kukuhudumia
hivyo wapewe moyo,"amesema.
Amewapongeza na kuwashukuru Wauguzi kwa kazi kubwa
walioifanya wakati wa wimbi la ugonjwa wa Corona na amewataka kuendelea
kutimiza wajibu wao na kuokoa maisha ya watu.
Akijibu hoja zilizowasilishwa na Wauguzi katika
risala yao, Waziri Ummy amesema suala la muundo linafanyiwa kazi na lilishawasilishwa Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa hatua zaidi.
Mhe. Ummy amesema kwa sasa Madaktari na wauguzi wafanye kazi kama timu moja ili kuleta matokeo chanya kwa jamii inayowategemea na hayo ya kiutawala yataendelea kuangaliwa na kufanyiwa kazi.
Baadhi ya Wauguzi walioshiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani Kitaifa Mkoani Manyara wakila kiapo cha uwajibikaji katika maadhimisho hayo
Kuhusu posho ya majukumu, amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itaangalia ni
namna gani inaweka mazingira bora kwa wauguzi walioko TAMISEMI kwa kadri
rasilimali zitakavyopatikana.
Ofisi yangu itahakikisha inatoa kipaumbele katika kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi wa Afya kwa kujenga nyumba za kutosha ili watumishi hao waweze kukaa kwenye vituo vyao na kufanya kazi kwa amani
Katika hatua nyingine, Mhe. Ummy ametoa zawadi ya sh.500,000 kwa Muuguzi Aldolefina Shayo wa Zahanati ya Kilangare iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same ambaye amevunja rekodi ya kuhudumia wagonjwa hamsini kwa siku bila kunung’unika na leo ameshindwa kushiriki maadhimisho hayo kwa kuwa yuko peke yake kwenye zahanati hiyo na hakuna mtu wa kumsaidia.
Waziri Ummy amesema katika ajira mpya zilizotangazwa
watapelekwa wauguzi wawili na Mganga mmoja ili kuboresha zaidi huduma za
Zahanati hiyo.
0 Comments