WAZIRI DKT.NDUMBARO : TEMBO ZAIDI YA 200 WAPO NJE YA HIFADHI YA MWL.NYERERE

 



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas akizungumza na Wananchi
 wa Kijiji cha Kitanda kilichopo katika wilaya ya Namtumbo

📌MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt Damas Ndumbaro ametoa tahadhari kwa Wakazi wa Ruvuma kuwa  tembo zaidi ya 200 wapo nje ya Hifadhi Taifa ya Mwl.Nyerere kutokana na Wafugaji kuingiza makundi ya ng'ombe ndani ya Hifadhi hiyo.

Dkt. Ndumbaro  ametoa tahadhali hiyo hususania kwa wakazi wa wilaya  Tunduru na Namtumbo wakati alipotembelea vijiji sita vilivyoathiriwa zaidi na tembo ili kukutana na wananchi na kujibu kero mbalimbali zinazotokana na uvamizi wa tembo katika maeneo yao wakitokea Hifadhi ya Taifa ya Mwl.Nyerere.

Amesema Wenyeviti wa Vijiji wamekuwa wakiwakaribisha  Wafugaji kutoka katika mikoa mbalimbali kuhamia katika maeneo ya vijiji hivyo na makundi makubwa ya ng'ombe na kisha kuingiza mifugo hayo ndani ya Hifadhi kwa ajili ya kupata malisho.

Amesema kwa mujibu wa utafiti wa Satelite uliofanyika hivi karibuni umeonesha tembo zaidi 200 wapo nje ya Hifadhi, Hivyo amewatahadharisha wananchi kutoa taarifa haraka pindi wanapoona makundi ya tembo yakiwa karibu kwenye makazi yao.

Baadhi ya Maaskari Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu wakiwa wamesimama mbele ya Wananchi ili waweze kuwafahamu ili pale tembo wanapotokea waweze kupoigiwa ili waweze kufika kwa ajili ya kutoa msaada wa kuweza kuwaondoa tembo hao kabla hawajaleta madhara kwa wananchi


Amesema kufuatia ng'ombe hao kuingia ndani ya Hifadhi wamekuwa wakilazimika kutoka nje ya maeneo yao kwa sababu tembo hawapendi kuchangamana na ng'ombe kutokana na harufu ya madawa wanayotumia kuoshewa wakiwa katika majosho.

Kutokana na  hali hiyo, Waziri Dkt.Ndumbaro ameagiza  ng'ombe walioingizwa ndani ya Hifadhi hiyo wafugaji walipe faini na ng'ombe hao wataifishwe na wasipouzika wapewe magereza kwa ajili ya chakula cha Wafungwa.

Aidha, Waziri Ndumbaro ametaja sababu nyingine iliyochangia Tembo kutoka nje ya Hifadhi kuwa ni tabia ya baadhi ya Wananchi kulima kwenye kingo za Hifadhi hali inayowavutia tembo kutoka nje kwa ajili ya kula mazao hayo.

Amesema idadi ya mashamba pamoja na wananchi kujeruhiwa inazidi kuongezeka siku hadi siku si kwa sababu idadi ya tembo imeongezeka bali ni kutokana na idadi ya watu kuongezeka na kulazimika kufanya shughuli ndani ya Hifadhi.

Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro amewaonya Wananchi kuacha kulima katika Jumuiya ya  Hifadhi ya Wanyamapori ya Wananchi kuwa hali hiyo imechangia tembo kutoka nje ya Hifadhi kula mazao.



Mbunge wa Namtumbo Mhe.Vita Kawawa akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kitanda ambapo amemueleza Mhe.Waziri Ndumbaro kuwa jumla ya Wananchi 36 pamoja na mashamba 63 ya mazao  yameathiriwa na Wanyamapori wakali na waharibifu 

Awali  akieleza kuhusu kero za wananchi wa jimbo lake la Namtumbo  Mhe. Vita Kawawa, amesema kuwa wananchi wa Jimbo lake la Namtumbo  kwa muda mrefu sasa wamekuaa wakiathiriwa na tembo wanaovamia makazi na mashamba yao na kumuomba  Waziri wa Maliasili na Utalii kuharakisha kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa Wananchi waliopata adha zitokanazo na adha ya tembo.

Kwa upande wa Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Hassan Kungu amemuomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Ndumbaro kuongeza fedha za vifuta jasho na vifuta machozi kwa sababu fedha wanayolipwa wananchi wake hailingani na thaman ya mashamba waliyoharibiwa na tembo

 



Post a Comment

0 Comments