📌MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu, Wizara ya
Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo, amewataka
wahandisi nchini kujiendeleza kitaaluma na kuongeza ujuzi mara kwa mara ili waweze
kulisaidia Taifa katika utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa na ya
kimkakati nchini.
Amesema hayo leo Jijini
Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa miradi kwa wahandisi
yalioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB).
Malongo ameipongeza
Bodi hiyo kwa utaratibu wa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wahandisi na
kuwataka kuendeleza utaratibu huo ambao unawajenga kitaaluma na kimaadili uwe
endelevu.
Aidha amezungumzia umuhimu
wa Bodi hiyo kuanzisha mfuko maalum wa wahandisi utakaowawezesha kuwajengea
uwezo wahandisi kiuchumi na hivyo kumudu kuwaendeleza.
Hakikisheni mnatembelea miradi mikubwa inayoendelea nchini ili kujifunza changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi
Mhandisi Malongo.
Naye mwenyekiti wa Bodi
ya ERB, Mhandisi Ninatubu Lema, amesema wahandisi wamejipanga kuhakikisha Sekta
ya Ujenzi nchini inaimarika na hivyo watashirikiana na Serikali ili kuhakikisha
miradi inayojengwa inawiana na thamani ya fedha.
Kwa upande wake Msajili
wa Wahandisi, Mhandisi Patrick Barozi, amesema mafunzo ya usimamizi wa miradi
yataendelea kutolewa ili kuimarisha uwezo wa wahandisi nchini na kuwataka wahandisi
wenye sifa kujisajili na Bodi hiyo.
Zaidi ya wahandisi elfu
30 wamesajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), katika fani mbalimbali hapa nchini na
mafunzo hayo yatawawezesha wahandisi hao kubobea kwenye fani zao na kuongeza
ubunifu kwenye utekelezaji na usimamizi wa miradi katika maeneo yao.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
0 Comments