📌RAMADHAN HASSAN
KUTOKANA na athari za mafuriko katika Kata ya Nkuhungu
Jijini hapa,Mkoa wa Dodoma umejipanga kuchimba na kujenga mitaro miwili mikubwa
ambapo mmoja utatiririsha maji kutoka kwenye mabwawa hayo na mwingine
utakaokinga maji ya mtiririko pembezoni mwa barabara kuu ya Dodoma kwenda
Singida.
Hatua hiyo imekuja kufuatia wakazi wa mitaa ya
Bochela,Salama,Mtube na Mnyakongo katika Kata ya Nkuhungu Jijini hapa kukumbwa
na mafuriko hali ambayo imesababisha kukimbia nyumba zao na hivyo kuishi
kwa majirani,ndugu jamaa na marafiki huku wengine wakiishi katika shule ya Msingi
Mnyakongo.
Kutokana na hali hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dk.Binilith
Mahenge amefika leo Jumapili,Mei 9 katika eneo hilo akiwa na Kamati ya
ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Josephat
Maganga na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,Antony Mavunde.
Akiwa katika eneo la tukio pamoja na wakazi waliathirika na
mafuriko hayo RC Mahenge amepokea taarifa ya kikosi kazi alichokiunda
ya hali halisi ya mafuriko na mapendekezo ya kutatua changamoto hiyo.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa hiyo,Mkuu huyo wa
Mkoa wa Dodoma,amesema wataalamu wameshauri maji yaliyopo katika eneo hilo
yanatakiwa kupunguzwa kwa kujengwa mitaro miwili mikubwa ambapo mmoja
utatiririsha maji yatakayozidi kutoka kwenye mabwawa hayo na mwingine utakaokinga
maji ya mtiririko pembezoni mwa barabara kuu ya Dodoma kwenda Singida.
“Hamu yetu tungetaka sana kuwarejesha wananchi katika
makazi yao lakini wataalamu wanashauri kwamba kitu cha kwanza lazima tuyazuie
maji yanayoingia hapa kutahitajika kujenga mtaro kutoka pale shell mtaro
mkubwa.
“Pili wanapendekeza lazima tutengeneze mtaro kutoka kwenye
bwawa kwa sababu hapa tupo chini kiwango cha mita tano kwahiyo ni kazi kubwa na
ni ya gharama hatuna uhakika itazuia maji kiasi gani,”amesema.
Amesema Serikali imejipanga kupeleka mapendekezo hayo
Serikalini ambapo kesho,Mkuu huyo wa Mkoa anatarajia kukutana na
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa kwa ajili ya kuzungumzia jambo hilo pamoja na
kuomba fedha.
“Kwahiyo tunasema hapa lazima tuandae namna ya kuwasaidia
wananchi wetu tunasema kwanza Serikali imejipanga na tutapeleka haya
mapendekezo lakini ujenzi wake hauwezi kukamilika mpaka Decemba tunahitaji
kuomba fedha,”amesema.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema wakati mipango hiyo ikiendelea Serikali ya Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Jiji la Dodoma imetoa zaidi ya viwanja 500 katika maeneo ya Nala na Mahomanyika kwa ajili ya waathirika hao vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili bure kwa wakazi hao.
Amesema pamoja na kuwapa viwanja mbadala hakuna mwananchi
yeyote ambaye atanyang’anywa eneo lake lilozingirwa na maji.
0 Comments