📌NTEGHENJWA HOSSEAH, OR-TAMISEMI
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), imepata kibali cha ajira za walimu wa shule ya msingi na sekondari
6,949 na kada mbalimbali za afya 2,726 watakaoajiriwa chini ya Mamlaka za
Serikali za Mitaa nchini.
Maombi ya ajira hizo yataombwa kwa njia ya mtandao
kuanzia Mei 9 hadi 23, mwaka huu kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ummy Mwalimu, amesema ajira hizo zitajaza nafasi
zilizoachwa wazi na watumishi waliokoma utumishi kutokana na sababu mbalimbali.
Serikali imetoa kibali, maana mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza kwamba atatoa ajira 6000 kwa walimu tulikuwa tunapata msukumo mkubwa kutoka kwa wananchi wakihoji kwanini TAMISEMI hatutangazi, taratibu za serikali lazima tupate kibali Menejimenti ya Utumishi wa umma.
Waziri Ummy
Hata hivyo, amesema serikali imetoa fursa kwa
waombaji ambao ni walemavu kutuma maombi yao kwa nakala ngumu na yaeleze aina
ya ulemavu wao na picha zao na kutumwa kwa anuani ya Katibu Mkuu TAMISEMI na
Ofisi ya Waziri Mkuu ili aione Mkurugenzi wa kitengo cha watu wenye ulemavu.
Akitaja sifa za waombaji wa ualimu, Waziri Ummy
amesema kwa shule ya msingi wanatakiwa walimu wenye daraja la IIIA kuwa
astashahada ya elimu ya msingi, elimu ya michezo, elimu ya awali na elimu
maalum.
“Mwalimu wa daraja la IIIB anatakiwa kuwa mhitimu wa
stashahada ya ualimu wa elimu ya awali, msingi, elimu maalum na Mwalimu wa
daraja la IIIC, mhitimu wa shahada ya ualimu masomo ya lugha ya kiingereza,
historia na jiografia,”amesema.
Kadhalika, amesema kwa shule za sekondari wapo kwenye makundi manne ambapo anatakiwa mwalimu wa daraja IIIB ambaye amehitimu stashahada ya ualimu wa masomo ya Fizikia, Hesabu, Baiolojia na Kemia.
“Pia mwalimu wa daraja IIIC ambaye amehitimu ualimu
aliyesomea elimu maalum kwa masomo hayo na shahada ya ualimu wa masomo hayo,
pia awe amehitimu stashahada ya uzamili katika elimu lazima awe mwenye shahada
ya kwanza yenye masomo tajwa,”amesema.
Pia amesema kwa waombaji wa ajira hizo ambao
wamesomea elimu ya sekondari nje ya nchi wanatakiwa kupata namba ya ulinganifu
wa matokeo inayoanzia na herufi EQ…kutoka Baraza la Mitihani la Tanznaia ili
kuingia kwenye mfumo wa maombi ya ajira.
“Pia wanatakiwa kupata ithibati ya masomo yao kutoka
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ili vyeti vyao vitambulike na kupata uhalali
wa kutumika nchini,”amesema.
Pamoja na hayo, Ummy amesema kada za afya ambazo
serikali itaajiri ni daktari daraja la II, daktari wa meno daraja la II, tabibu
daraja la II, tabibu msaidizi, tabibu wa meno daraja la II, tabibu meno msaidizi,
mfamasia daraja la II.
Nyingine ni mteknolojia wa dawa daraja la II,
mteknolojia msaidizi wa dawa, mteknolojia wa maabara daraja II, mteknolojia
msaidizi maabara, mteknolojia mionzi daraja la II, mteknolojia msaidizi wa
mionzi, mteknolojia wa macho daraja la II.
Kadhalika, alisema itaajiri Ofisa Muuguzi daraja la
II, Ofisa muuguzi msaidizi daraja la II, Muuguzi daraja la II, mtoa tiba kwa
vitendo daraja la II, Ofisa afya mazingira daraja la II, Ofisa afya mazingira
msaidizi daraja la II, Msaidizi wa afya, Katibu wa afya daraja la II, Ofisa
ustawi wa jamii daraja la II na Ofisa lishe daraja la II.
Amesema ajira zitatolewa kwa haki na hataruhusu
kuwepo na aina yeyote ya ushawishi na
kusisitiza watazingatia wale waliomba kwa maelekezo yaliyotolewa.
0 Comments