RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan amewasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo
Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya kuanza ziara rasmi ya siku mbili kufuatia
mwaliko wa mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Alipowasili jijini Nairobi Mhe. Rais Samia
alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Raychelle Omamo na Waziri wa Michezo, Utamaduni
na Urithi Mhe. Amina Mohammed.
Baada ya kuwasili Mhe. Rais Samia aliekea
hotelini kwa ajili ya mapumziko kidogo na baadaye alielekea Ikulu ya Nairobi
kwa ajili ya kupokelewa rasmi na Mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta ambapo
alikagua gwaride na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake.
Akiwa Ikulu jijini Nairobi Mhe. Rais alifanya mazungumzo
ya faragha na mwenyeji wake Mhe. Rais Kenyatta na baadaye walifanya mazungumzo
rasmi ambayo yalihudhuriwa na wajumbe wa pande zote mbili.
Baada ya kumaliza mazungumzo yao viongoazi hao
walizungumza na waandishi wa habari na baadaye Mhe. Rais Samia alikwenda kuweka
shada la maua katika Kaburi la Baba wa Taifa la Kenya hayati Mzee Jomo
Kenyatta.
Jioni Mhe. Rais atahudhuria dhifa ya Kitaifa
ambayo imeandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta.
Kesho tarehe 05/05/2021 Mhe. Rais akiwa na
mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta atahutubia Mabunge ya Kenya na baadaye
atafungua Kongamano la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania linalofanyika
jijini Nairobi.
0 Comments