📌MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar Mhe. Dk. Hussein Mwinyi akutana na
Mchezaji wa Crystal Palace, Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi ameipongeza azma ya Mchezaji wa timu ya mpira wa miguu wa
Klabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL) Mamadou Sakho
ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana hapa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo Ikulu Jijini
Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mchezaji wa timu ya mpira
wa miguu wa Kilabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL)
ambaye pia ni Mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Mamadou Sakho.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba
azma hiyo ni mwanzo mzuri katika kuinua na kuendeleza vipaji vya michezo vya
vijana wa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Mamadou kwa kuitembelea
Zanzibar kwa mara ya pili kutokana na mazingira pamoja na watu wa Zanzibar na
utamaduni wao.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza mchezaji huyo wa timu ya
Crystal Palace kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana
nae katika kuanzisha kituo hicho cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana
hapa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alimueleza mchezaji huyo kuwa ujio wake
una umuhimu mkubwa katika kuutangaza utalii wa Zanzibar pamoja na vivuto
vilivyopo.
Nae Mchezaji wa timu ya mpira wa miguu wa timu ya
Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL) ambaye pia ni Mchezaji
wa timu ya taifa ya Ufaransa Mamadou Sakho alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma yake
ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana hapa Zanzibar.
Mamadou ambaye amefuatana na Mkewe Majda Sakho, alisema
kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya
michezo kwa vijana hapa Zanzibar kwa kutambua kwamba ana deni na wajibu mkubwa
wa kuleta maendeleo Afrika akijuwa kwamba yeye ni Mwafrika licha ya kwua
amezaliwa Ufaransa na anabeba uraia wa Taifa hilo.
Aliongeza kuwa ameichagua Zanzibar kuwa ni eneo maalum kwa
kuanzisha kituo hicho kitakachoendeleza soka hapa nchini.
0 Comments