📌RHODA SIMBA
BEI za bidhaa za vyakula imeongezeka na kusababisha Mfumuko wa bei ya Taifa kupanda hadi kufikia asilimia 3.3 kutoka 3.2 kwa mwezi Machi mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ruth Minja ametaja bidhaa zilizoongezeka bei kuwa ni Ngano kwa asilimia 8.9, Nyama 4.2, Samaki wabichi 28.1, Dagaa22.0, Mafuta ya kupikia 24.6, Matunda kwa asilimia 24.6.
Ruth ametaja bidhaa nyingine zilizopanda bei kuwa ni Viazi Mviringo kwa asilimia 5.7, Viazi vitamu 14.7, Ndizi za kupika 7.6 Maharage 6.4, na Mihogo Mikavu asilimia 4.2.
Amesema mfumuko wa Bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi machi mwaka huu umeongezeka kutoka asilimia 4.2 mwezi februari hadi asilimia 4.8.
Mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula visivyochakatwa ,nishati na bili za maji(Core inflation) kwa mwezi Machi mwaka huu umebaki kuwa asilimia 3.6 kama ilivyokuwa mwezi februari mwaka huu.
HALI ILIVYO SOKONI.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Majengo Hamisi Juma amesema upatikanaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara umeendelea kuwa wa uhakika hivyo kupelekea baadhi ya bidhaa kuendelea kushuka bei.
Amesema kwa mwaka huu mfuko wa bei haujatokea mkubwa ukilinganisha na mwezi kama huu mwaka jana.
Hivi sasa ukienda soko la Majengo zile bidhaa za msingi kama vile mchele, unga wa ugali, maharagwe na vitunguu bei zake zimekuwa stimilivu ukilinganisha na mwaka jana miezi kama hii ambapo zilikuwa juu
“Mchele sasa hivi bei yake ni kuanzia 2000 kushuka chini wakati mwaka jana miezi kama hii Ilikuwa 2500, pia unga wa ugali bei yake sasa ni 1200 kushukachini wakati mwaka jana ilifika hadi 2600 na maharage bei yake ni 2400 ukilinganisha na mwaka jana miezi kama hii ambapo bei ilipanda hadi kufikia 2800,”ameeleza
Kwa upande wake Mfanyabiashara Anitha Saimoni amesema elimu kuhusu mfumuko wa bei inabidi itolewe kwa wafanyabiashara hiyo itasaidia kukomesha tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei bila utaratibu.
Amesema kumekuwa na kasumba kwa wafanyabiashara wasio waaminifu kupandisha bei za baadhi ya bidhaa bila sababu au utaratibu maalumu.
Elimu kuhusu mfumuko wa bei ikitolewa kwa wafanyabiashara itasaidia kukomesha tabia ambayo sio nzuri na haipendezi inayofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei hovyo.
SOMA HII PIA: SERIKALI YATOA VIWANJA 566 KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO DODOMA
0 Comments