📌MWANDISHI WETU
NAIBU
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme
(TEMESA), kuhakikisha wanayatoa magari yote yaliyotelekezwa na wamiliki wake
katika karakana zote nchini na kusababisha mrundikano ndani ya karakana hizo.
Akizungumza na
Menejimenti ya Wakala huo, jijini Dodoma, Waitara amesema kuwa hatua hiyo
itapelekea kupunguza msongamano katika karakana hizo na hivyo kupatikana kwa
nafasi ili kuruhusu magari mengine kupata huduma kiurahisi.
Magari hapa ni mengi na mlundikano ni mkubwa, mengine yanaonekana ni ya muda mrefu, hakikisheni mnayatoa na kuyapeleka kwa wenyewe ili kupunguza msongamano hapa na hata katika karakana zenu nyingine nchi nzima
Waitara.
Aidha, Waitara ameutaka
Wakala huo kuboresha huduma zao nchi nzima ikiwemo kutatua mianya yote
inayopelekea uhujumu na kupelekea utendaji wa kusuasua kwa watumishi wa Wakala
huo.
“Hakikisheni kuwa
mnapunguza gharama, mnatumia muda mfupi na vipuri sahihi katika utengenezaji wenu
wa magari, mkifanya hivi mtapunguza malalamiko kutoka kwa washitiri wenu”,
amesisitiza Waitara.
Aidha, ameagiza Wakala
huo kuhakikisha wanatafuta njia sahihi ya kuhifadhi mafuta machafu
yanayomwagika wakati wa utengenezaji wa magari ili kuhifadhi mazingira katika
maeneo yao ya kazi.
Kuhusu suala la vivuko,
Waitara ameutaka Wakala huo kuhakikisha kila kivuko kinajisimamia na
kujiendesha kwa faida na kutaka Wakala huo kupitia upya tozo za nauli za vivuko
nchini katika baadhi ya maeneo bila kuumiza wananchi.
“Huduma za Serikali
hazitakiwi kufanywa kwa kubahatisha, kwa mfano katika Kivuko cha Nyamisati
utaratibu wa safari na nauli haueleweki, wananchi wa huko wanalalamika sana,
kaeni mlirekebishe hili, Serikali haitaki watu wababaishaji”, amefafanua Naibu
Waziri huyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi
na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakati akikagua moja ya vifaa vya kisasa vya
matengenezo ya magari ya Serikali vilivyopo katika Karakana ya Wakala huo
jijini Dodoma.
Ametaja changamoto
nyingine kuwa ni uchakavu wa miundombinu na vifaa vya karakana ambapo amesema
kuwa karakana hizo zimejengwa miaka mingi iliyopita hivyo kuhitaji ukarabati
mkubwa.
Kwa upande wake, Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Heriel Mteri, amesema kuwa Wakala unakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo wakala kuendesha baadhi ya vivuko vyenye mapato
madogo na hivyo kushindwa kujiendesha vyenyewe na kupelekea Wakala kutoa ruzuku
ya kuviendesha.
Ameongeza kuwa, kwa
sasa Wakala unatumia mfumo wa kisasa wa kubaini vipuri ambavyo sio halisi katika
karakana zake zote ili kudhibiti udanganyifu ambao unafanywa na baadhi ya
wafanyabiashara.
Naibu Waziri Waitara,
amefanya ziara TEMESA jijini Dodoma, ili kujionea utendaji wa wakala huo na
kuzungumza na Menejimenti kuhusu namna
ya kuboresha huduma katika Wakala huo.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
0 Comments