📌MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewataka watendaji wa Sekta ya Uchukuzi na Taasisi zake kuhakikisha wanajali watumishi kwa kusimamia kanuni, taratibu na sheria ili kupata matokeo chanya katika utendaji.
Akizungumza mara baaada ya kufunga Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi jijini Dodoma, Naibu Waziri huyo amesema ufanisi wa taasisi unakwenda sanjari na kusimamia vizuri maslahi, matumizi bora ya fedha yanayozingatia taratibu, ushirikishwaji na utii kwa Mamlaka.
Hamuwezi kufanikiwa kama katika taasisi zenu kila mmoja anakwenda njia anayotaka. Lazima mjifunze kuheshimu Mamlaka zilizopo, mjali maslahi ya watumishi, muwashirikishe katika ngazi zote, mkifanya hivyo wala hamtatumia nguvu kusimamia Taasisi na matokeo yataonekana
Naibu Waziri Waitara
Naibu Waziri Waitara ameongeza kuwa Serikali imejiwekea malengo ya kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati hivyo ni lazima wakuu wa Taasisi wapate taarifa sahihi za kila siku za maendeleo ya miradi hiyo ili kuwa na kauli moja kuanzia ngazi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wasimamizi.
Aidha, Naibu Waziri Waitara amezitaka taasisi zote zinazokusanya mapato kuhakikisha zinapeleka gawio Serikalini ili fedha hizo zitumike kuendeleza miradi mingine na kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwatumikia wananchi kwa kuwapatia miundombinu bora.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi Gabriel Migire, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa wataalam wa Sekta wamejipanga kwa kuweka programu maalum ya ukaguzi wa miradi kila mwezi ili kuona maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji.
Migire, amesema kuwa sekta iko tayari wakati wote kutoa ushirikiano kwa viongozi kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi kwa kutoa taarifa sahihi hususani kwenye utoaji wa majibu kwa maswali yanayoulizwa bungeni.
Baraza
la Wafanyakazi la Sekta ya Uchukuzi limekaa kwa siku mbili ambapo pamoja na
mambo mengine limejadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/21 na mpango
wa bajeti kwa mwaka 2021/22.
0 Comments