📌FARIDA RAMADHANI -WFM
SERIKALI ya Tanzania imepokea nyongeza ya kiasi cha
Euro milioni nne kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji mkoani Kigoma kutoka
Serikali ya Ubelgiji.
Hafla fupi ya utiaji saini wa mkataba wa marekebisho
ya nyongeza ya mradi huo ilifanyika jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha na Mipango ambaye pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel
Tutuba kwa upande wa Serikali na Balozi wa Ubelgiji nchini, Bw. Peter Van
Acker.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba alisema mradi huo ambao ulianzishwa
kwa ajili ya Wilaya zote sita za Mkoa wa Kigoma, mwanzoni ulitarajiwa kugharimu
Euro milioni nane.
Sasa hizi Euro milioni nne zitakwenda kuongezea na kufanya jumla ya Euro milioni 12 sawa na takribani Shilingi bilioni 33 za kitanzania ambazo zitatumika kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini na mijini mkoani humo
Emmanuel Tutuba
Amesema katika Mkoa wa Kigoma, Serikali ya Ubelgiji
pia imefadhili mradi mwingine wa kilimo ambao unaendelea na umegharimu Euro
milioni nane sawa na takribani Shilingi bilioni 22, hivyo miradi yote miwili
(mradi wa maji na kilimo) inagharimu jumla ya takribani Shilingi bilioni 55.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba (kushoto) na Balozi wa Ubelgiji, Mhe. Peter Van Acker, wakisaini mkataba huo |
Aidha ameipongeza Serikali ya Ubelgiji kwa kubuni njia nzuri ya kupunguza gharama za utekelezaji wa mradi wa kilimo kwa kujenga madaraja ya mawe ambayo yanaweza kuunganisha sehemu ya mashamba na sehemu ya makazi na kupunguza gharama za ujenzi wa daraja moja kwa takribani asilimia 80.
Bw. Tutuba aliihakikishia Serikali ya Ubelgiji kuwa fedha
hizo zitatumika kikamilifu na utekelezaji wa miradi hiyo utakamilika kwa
wakati.
Naye Balozi wa Ubelgiji nchini, Bw. Peter Van Acker
amesema Serikali ya nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania kwa kuendelea
kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema anaamini mradi wa maji mkoani Kigoma utatatua
changamoto ya maji mkoani humo na ameahidi kuwajibika katika masuala ya maji
kama hotuba ya Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan ilivyosisitiza.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba (kushoto) na Balozi wa Ubelgiji, Mhe. Peter Van Acker, wakibadilishana mkataba |
Akipokea kwa shukrani nyongeza hiyo, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, aliishukuru Serikali ya Ubelgiji kwa
kuendeleza ushirikiano mzuri na Tanzania na kubainisha utekelezaji wa mradi wa
maji mkoani Kigoma utanufaisha watu takribani laki moja na 30.
Ameahidi kusimamia matumizi ya fedha hizo kikamilifu
ili kuhakikisha malengo ya utekelezaji wa mradi huo yanatimia kwa wakati.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango – Dodoma)
0 Comments