📌WIZARA YA KILIMO
SERIKALI imesema ni
marufuku kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuongeza bei elekezi
ya mbolea bali ihakikishe wakulima wanapata mbolea bora na kwa wakati.
Waziri wa Kilimo
Profesa Adolf Mkenda ametoa agizo hilo leo (16.04.2021) jijini Dodoma wakati alipofungua kikao kazi
cha Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania kufuatia maombi
yaliyowasilishwa na bodi kwa wizara.
Bei elekezi ya mbolea sitoongeza licha ya maombi kuletwa wizarani. TFRA nawataka mhakikishe bei ya mbolea iliyopo sasa inaendelea na wakulima wapate mbolea yenye ubora na kwa wakati ili watumie kuzalisha mazao ya Kilimo.
Profesa Mkenda.
Profesa Mkenda
aliongeza kusema lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuona gharama za
uzalishaji wa mazao zinashuka ili wakulima waongeze tija kwa kupata mbolea na
pembejeo zingine kwa bei rahisi hatua itakayowafanya wakuze kipato chao na
uchumi wa nchi kukua.
Ameitaka bodi ya
wakurugenzi wa mamlaka ya udhibiti wa mbolea kukutana na wafanyabiashara na
wamiliki wa viwanda vya kuzalisha mbolea kujadili na kuweka mikakati ya kufanya
wakulima wapate mbolea bora na kwa bei rahisi.
Katika hatua nyingine
Prof. Mkenda ameagiza mamlaka hiyo kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
(TARI) kutoa elimu ya upimaji afya ya udongo kwa wakulima ili watambue aina ya
udongo unaofaa kwa aina gani ya mbolea lengo waweze kuongeza tija kwenye
uzalishaji wa mazao.
Waziri huyo wa Kilimo
alibainisha kuwa hali ya upatikanaji mbolea nchini umefikia tani 631,660 mwaka
huu Februari kati ya mahitaji ya tani 718,051 na kuwa serikali itaendelea
kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini ili kupunguza utegemezi
wa mbolea toka nje ya nchi.
Kwa upande wake
Veronica Soko mjumbe wa bodi ya TFRA anayewakilisha wakulima wadogo kupitia
MVIWATA almeiomba serikali kuweka utaratibu wa kuvikopesha vyama vya ushirika
wa wakulima ili wanunue mbolea kwa mfumo wa pamoja hatua itakayosaidia wakulima
kupata kwa bei nafua.
Mkulima huyo wa mpunga toka Madibira wilaya ya Mbarali alibainisha kuwa wanachama wake wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa njia ya umwagiliaji na matumizi ya mbegu na mbolea bora kuongeza uzalishaji toka gunia 20 hadi 25 kwa hekta hadi kufika tani 7 hadi 10 mwaka 2019.
Vyama vya ushirika
vikitumika kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja itasaidia wakulima kufikishiwa
bidhaa hiyo kwa bei nafuu huku ikiwa iezingatia aina ya zao wanalozalisha. Veronica Soko.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA Prof. Anthony Mshandete ameipongeza serikali kwa maelekezo ambayo imekuwa ikiyatoa hatua ianayosaidia bodi yake kuwafikia wakulima wengi kwa kufikisha mbolea inayohitajika kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja( BPS).
Prof. Mshandete amesema
bodi hiyo ilioanzishwa kwa Sheria ya
Mbolea Namba 9 ya mwaka 2009 itaendelea kuhakikisha inadhibiti ubora wa mbolea
ili wakulima wanufaike na kuwezesha
Kilimo kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa .
Mkakati wetu ni kuhamasisha watanzania wengi waanzishe viwanda vya mbolea hapa nchini hali itakayosaidia kupata mbolea bora na yenye gharama nafuu hivyo kuachana na utegemezi wa mbolea toka nje ya nchi.
Prof. Mshandete.
Takwimu za Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea Tanzania zinaonesha katika mwaka 2020 Tanzania imetumia Dola
za Kimarekani Milioni 229.8 kuingiza nchini mbolea tani 659,197 toka nje ya
nchi.
UMEISOMA HII?👇👇👇
0 Comments