MWENYEKITI CCM DODOMA :KATIBA YA MWAKA 1977 BADO INA NGUVU, HAINA HAJA YA KUCHOKONOLEWA


📌RHODA SIMBA

HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma imeazimia kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 bado ina nguvu,hivyo hakuna ulazima wa kuichokonoa kwa kutafuta Katiba mpya hasa ile pendekezwa.

Maazimio hayo yamepitishwa leo jijini hapa katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoani Dodoma,ambapo pamoja na mambo mengine pia kimempongeza Rais wa Tanzania Mh,Samia Suluhu Hassan kwa kushika nafasi ya juu  ya uongozi nchini.

Aidha akiongea katika kikao hicho Mwenyekiti wa CCM mkoa  Godwin Mkanwa amesema katika siku  37 alizokaa madarakani nchi imetulia na mambo yote  yanaenda kama yalivyo pangwa na miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa.

"Ni maoni ya Halmashauri kuu kuwa si nchi zote zingeweza kupita na kuwa salama katika mazingira magumu ya kuondokewa na kiongozi mkuu wa nchi  na nchi kubaki salama, hivyo halmashauri kuu ya CCM ya mkoa wa Dodoma inaona katiba yetu ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 bado ina nguvu na imefanikiwa kutupitisha salama katika kipindi kigumu ni kipimo cha kwanza na cha wazi kwa katiba yetu"  Mkanwa.

Hata hivyo amesema halmashauri kuu ya CCM ya mkoa wa Dodoma imeona katiba hiyo bado inafaa na hakuna ulazima wa kuibadilisha kwa kutafuta katiba mpya wakati iliyopo bado inafaa.

Mathalani Katiba pendekezwa kwenye jambo hili ilikuwa inasema Rais akifariki zikipita siku 90 uitishwe uchaguzi wa kujaza nafasi hivyo halmashauri kuu ya mkoa wa dodoma inaona kama Katiba pendekezwa ingekuwa ndiyo Katiba inayotumika isingetutoa salama mpaka tukawa kama hivi tulivyo leo

Mkanwa.

Sambamba na hayo ametoa wito kwa watanzania wote kwa umoja kuunga mkono serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kuwataka wafanye kazi kwa bidii  na kulipa kodi ili nchi iweze kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii.

Maazimio hayo yanajiri wakati ambapo chama cha mapinduzi CCM) kikitarajia kufanya mkutano wa chama hicho April 30.


Post a Comment

0 Comments