Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akikagua mitambo ya kufua hewa tiba (Oksijeni) iliyosimikwa Kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma |
📌CATHERINE SUNGURA-WAMJW
SERIKALI
imeweza kujibu changamoto za wataalamu wa afya katika hospitali saba za
rufaa za mikoa ili kuwahudumia kwa ufanisi wagonjwa wa dharura kwa
kuimarisha kwa kusimika mitambo ya kufua hewa tiba (Oksijeni) na hivyo kupunguza
gharama za uendeshaji wa hospitali hizo na kuwezesha hospitali zingine za
halmashauri na vituo vya afya.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotembelea
hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma kujionea jinsi walivyounganisha mitambo hiyo
kwenye wodi ya wagonjwa mahututi na watoto.
Dkt.Gwajima amesema mitambo hiyo ambayo Serikali kwa
kushirikiana na Benki Kuu ya Dunia hivi sasa imefungwa kwenye hospitali za
rufaa za mikoa saba ya Dodoma, Mtwara ,Manyara, Mbeya, Amana Geita na Songea na
hivyo wizara yake ipo njiani kukamilisha kufungia hospitali zote za rufaa za
mikoa hapa nchini.
Mitambo hii imefungwa kwa gharama isiyopungua bilioni 1.4 kila hospitali na inalenga kuzalisha mitungi 200 ya hewa hiyo kwa masaa 24 , na kila mtambo unayo sehemu ya mabomba yenye mita 400 yanayosafirisha hewa hii pia mitungi 73 imenunuliwa pamoja na mitambo hii kwa hivyo, haya ni mapinduzi makubwa
Mmoja wa Wazazi wa Watoto waliolazwa Kwenye hospitali hiyo akiongea na Waziri wa Wizara ya Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotbelea wodi hiyo na kujionea jinsi Oksijeni ilivyounganishwa wodini
Aidha, Dkt. Gwajima amefurahishwa na uongozi wa
hospitali hiyo kwa kukamilisha kufunga
mitambo hiyo na kuanza kutoa
huduma kwenye wodi ya wagonjwa mahututi(ICU) pamoja na wodi ya watoto na hivyo
wameweza kuunganisha vitanda 78 kutoka
vitanda 10 vya awali na kufanya jumla ya vitanda 88 kupatiwa huduma hiyo
hospitalini hapo.
Hatua hii itapunguza kwa kiwango kikubwa gharama za kuhudumia mgonjwa mwenye mahitaji ya hewa hii. Wito wangu tuitumie vizuri na kuzingatia na kuhakikisha matengenezo kinga yanafanyika kwa ufanisi.
Dkt. Gwajima amesema kuwa uwekezaji huo umeweza
kujibu changamoto ya kipindi cha mlipuko
wa Covid-19 ulioripotiwa nchini mwezi
Machi mwaka 2020 na hivyo kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya hewa ya
oksijeni na kuwa gharama zake zilipanda.
“Niwapongeze sana waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa kwa kuja na wazo hili la kufunga mitambo hiyo kwenye hospitali zetu na hivyo tutaweza kusaidia hospitali za wilaya na vituo vya afya na hivyo kuwapunguzia matumizi ya fedha ya kununua oksijeni, haya ni mapinduzi makubwa kwa Serikali yetu”. Alisisitiza Dkt. Gwajima
Kwa upande kwa kuepuka magonjwa ya kuambukiza
ambayo yameanza kuyakumba mataifa
mengine, Waziri huyo aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wafawidhi kwenye
hospitali za rufaa za mikoa kuendelea kutoa elimu kwa umma kwa kutumia vyombo
vya radio vilivyopo kwenye maeneo yao (Community radio) ili kuwaondolea
wananchi hofu na kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na magonjwa ya
kuambukiza na yasiyoambukiza ikiwemo janga la Corona.
Serikali kupitia sekta ya afya kwa kushirikia na wadau wake nchini iko makini kufuatilia kinachoendela duniani na kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama na imara katika kudhibiti milipuko ya magonjwa mbalimbali ikiwemo huu wa Covid-19
Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima aliwakumbusha wadau,wataalam pamoja na
wananchi wote kuendelea kuchukua
tahadhari muhimu ambazo zimekuwa
zikielimishwa mara kwa mara dhidi
ya kujikinga na kudhibiti magonjwa
mbalimbali ikiwemo Covid-19 kwa kuepuka hofu, kuimarisha tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni, kufanya
mazoezi,kula lishe au vyakula vya
mbogamboga kwa wingi na matunda,kutumia tiba asili, kuepuka misongamano isiyo
ya lazima na mwisho kuwahi kwenye vituo
vya kutolea huduma za afya mara unapoona
dalili za maradhi yeyote.
Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa
Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema
wanatarajia kufunga mitambo ya
kujazia hewa tiba hiyo ili kuweza kusaidia vituo vya afya vilivyo jirani na
kusambaza huduma hiyo kwenye hospitali nzima.
0 Comments