📌WFM-DODOMA
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni
(Mb), amemuagiza Mhasibu Mkuu wa Serikali pamoja na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa
Serikali kuwasimamia ipasavyo wataalamu wa kada ya uhasibu nchini ili kukomesha
kasoro za kiuhasibu na upotevu wa fedha za umma unaobainishwa kila mara na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mhandisi Masauni alitoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa utiaji
Saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na
Bodi ya Uhasibu ya Kimataifa (ACCA) kwa ajili ya kuanzisha mafunzo ya uhasibu
wa ngazi ya kimataifa ACCA katika vituo vya chuo hicho kwenye mikoa ya Arusha,
Dar es Salaam na Dodoma.
“Taarifa ya CAG imeonesha udhaifu wa kimahesabu kwenye baadhi ya Taasisi
za Serikali na Halmashauri jambo ambalo halikubaliki, sisi wadau wa sekta ya
fedha tuna kazi kubwa ya kuendelea kukemea na kuwaelimisha wataalamu wa kada ya
uhasibu na wakaguzi katika kutimiza majukumu yao ili kuwaletea wananchi
maendeleo”, alisema Mhandisi Masauni.
Aidha, Mhe. Mhandisi Masauni alikipongeza chuo hicho kwa kupewa ithibati
ya kuwa Kituo cha Mafunzo ya Uhasibu wa Kimataifa na kuratibu mitihani ya
Taasisi ya ACCA itayowezesha chuo hicho kuratibu mafunzo hayo nchini.
Ni furaha yetu kuona sasa tutaweza kuzalisha wataalamu wengi zaidi wa uhasibu wa kimataifa kupitia Chuo chetu cha Uhasibu Arusha, pia chuo kitaweza kuongeza wigo wa kuanza kudahili wanafunzi kutoka nchi jirani
Mhandisi Masauni.
Alisema kuwa mpango huo utaongeza idadi ya wataalamu wenye sifa ya
uhasibu wa kimataifa na itaokoa fedha nyingi zilizokuwa zinatumika kuwasomesha
wataalamu nje ya nchi.
Mhe. Mhandisi Masauni aliongeza kuwa ni vizuri kuwajengea wataalamu
uwezo wa kushindana kimataifa lakini pia kwenda sambamba na viwango vya
kimataifa ambavyo hubadilika mara kwa mara kulingana na sayansi na teknolojia.
Naye Mhasibu Mkuu wa Serikali Bw. Francis Mwakapalila alisema kuwa
kuanzishwa kwa kituo cha mafunzo na udahili wa mitihani ya ACCA (CPA kwa
kiwango cha Kimataifa) kutaongeza wigo wa wataalamu nchini na hivyo kuboresha
uandaaji wa taarifa za uhasibu.
“Ujuzi na maarifa yatakayopatikana yatakuwa ni nyenzo muhimu itakayoongeza
ufanisi katika utendaji kazi na kuendeleza taaluma ya uhasibu na kuongeza idadi
ya wataalamu”, alisema Bw. Mwakapalila.
Alitoa rai kwa wote walio katika Taasisi za umma na binafsi kuchangamkia
fursa hiyo ili kupata weledi katika taaluma ya uhasibu na kuleta msukumo mkubwa
wa kukuza uchumi nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Eliamini Sedoyeka alisema kuwa
makubaliano hayo yatasaidia
wataalamu wa uhasibu kupata ujuzi na kutambulika kimataifa lakini pia kusaidia
kutoa mafunzo kwa gharama nafuu.
Baada ya muda mrefu sasa kumetokea mabadiliko mbalimbali katika sekta yetu hii na pia muingiliano wa masuala ya kimataifa. Lakini pia, umekuwa ni wakati mzuri wa kuhakikisha kuwa wataalam wetu wa uhasibu pia wanapata sifa za Kimataifa na kutambulika vyema katika ulimwengu tuliopo
Prof. Sedoyeka
Naye mwakilishi wa Bodi ya Uhasibu ya Kimataifa (ACCA) Bw. Jenard Lazaro
alisema kuwa chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kinachomilikiwa na Wizara ya Fedha
na Mipango, kinakuwa chuo cha tatu kwa nchi za Afrika ya Mashariki kutoa
mafunzo hayo na kusisitiza ushirikiano katika utekelezaji wa makubaliano hayo
ili kuendeleza fani ya uhasibu nchini.
Bodi hiyo ya ACCA yenye makao yake makuu nchini Uingereza ina wanachama
wapatao laki mbili huku hapa nchini ikiwa na wanachama 400 na wanafunzi zaidi
ya 2,000.
0 Comments