📌MWANDISHI WETU
KAMATI ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini imeeleza kuridhishwa kwake na Kanuni zinazosimamia
Sekta ya Madini na kueleza kuwa, marekebisho kidogo yaliyopo hayazuii Sekta
kufanya kazi.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula Aprili 17, 2021
jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya Kamati hiyo
kujengewa uelewa kuhusu Kanuni mbalimbali zinazosimamia Sekta ya Madini.
Amesema kuwa, upo
umuhimu wa Kamati hiyo kupatiwa elimu
kwani ndiyo inayofanya kazi kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na hivyo elimu hiyo itaiwezesha Kamati husika kuisimamia Sekta ipasavyo
ikiwemo kuisadia Serikali katika usimamizi wa Sekta ya Madini.
Tunapokutana kama hivi tunapata nafasi ya kuangalia ni namna gani Kanuni hizi zinafanya kazi, zinachangia vipi kwenye maendeleo na ukuaji wa sekta lakini pia tunapata nafasi ya kuona changamoto na kushauri Serikali namna ya kuzitatua.
Kitandula.
Katika Semina hiyo, Kamati hiyo ya Bunge imeelimishwa kuhusu Sheria ya Madini Sura ya 123 na Marekebisho yake yaliyofanyika Mwaka 2007, Kanuni mbalimbali zikiwemo Kanuni za Masoko ya Madini, Kanuni za Madini (Biashara ya Almasi) za Mwaka 2019, Kanuni za Madini (Udhibiti wa Eneo Tengefu la Mirerani ya Mwaka 2019 na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia).
Naye, Waziri wa Madini Doto
Biteko akizungumza katika Semina hiyo, amesema kuwa, kama nchi imepiga hatua
katika utekelezaji wa Matakwa 18 ya Kimataifa kuhusu Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali
Madini, Mafuta na Gesi Asilia na kueleza kuwa, ni
maeneo 7 tu kati ya 18 ambayo bado yanaendelea kutekelezwa na Wizara.
Kauli hiyo ya Waziri ni
ufafanuzi baada ya Kamati hiyo kutaka kujua ni kwa namna gani Serikali imetekeleza
matakwa ya Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta
na Gesi Asilia Tanzania (TEITA) ya Mwaka 2015.
Akizungumzia Semina
hiyo amesema inalenga kujenga uelewa wa pamoja ili kuiwezesha Kamati husika
kuifahamu vizuri sekta na hivyo kuishauri Wizara ipasavyo na hatimaye
kuiwezesha sekta kusonga mbele.
Akiwasilisha mada
kuhusu Sheria ya Madini Sura ya 123, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya
Madini Edwin Igenge, ameieleza Kamati hiyo kuhusu historia ya mabadiliko ya Sheria ya Madini kabla na baada ya Uhuru ikiwemo kubainisha mapungufu
kadhaa ambayo yalipelekea kufanyika kwa Mabadiliko Makubwa Mwaka 2017.
Igenge ameeleza kuwa, Mabadiliko
ya Mwaka 2017 yaliwezesha kutungwa kwa Sheria za Kulinda Maliasili za Nchi na hivyo kuwezesha umiliki wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa
wananchi chini ya usimamizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa niaba ya
wananchi.
Akiwasilisha kuhusu Kanuni za Masoko ya
Madini, Afisa Sheria Wizara ya Madini Damian Kaseko, ameileza Kamati hiyo
kuhusu masuala kadhaa ikiwemo taratibu za uanzishwaji wa masoko ya madini, namna
masoko hayo yanavyofanya kazi, utatuzi wa migogoro inayotokana na shughuli
katika masoko, utaifishaji wa madini kwa mujibu wa Kanuni za Masoko pamoja na
mambo mengine.
0 Comments