DKT. NDUGULILE AFUNGUA MKUTANO WA 41 WA SATA WA NCHI ZA SADC

 


📌FARAJA MPINA

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amefungua Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Sourthern Africa Telecom Association (SATA) ambapo nchi ya Tanzania kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imekuwa mwenyekiti wa Umoja huo.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma ambapo nchi 23 za umoja huo zimeshiriki Dkt. Ndugulile amezungumzia fursa mbalimbali zinazopatikana kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano hasa matumizi ya intanenti kuwa yanawezesha kufanyika kwa shughuli za biashara, uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Aidha, amesema kuwa ni vema elimu ya matumizi sahihi ya mtandao iendelee kutolewa ili kupunguza uhalifu wa mitandaoni na mmomonyoko wa maadili kulingana na tamaduni zetu za kiafrika ambao kwa namna moja ama nyingine unasababishwa na kukua kwa matumizi ya intaneti.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa anatamani kuona gharama za mawasiliano baina ya  nchi hizo za Afrika zinapungua kwa kutengeneza mfumo madhubuti wa kuwa na mawasiliano ya ndani ya Afrika (Regional Hub) badala ya kusafirishwa kwenda nchi za ulaya na marekani ndipo yarudi na kumfikia mlengwa.

Serikali imewezesha kuwa na mawasiliano ya ndani kama nchi hivyo kushusha gharama za huduma za mawasiliano ambapo miongoni mwa zinazofanya vizuri sana kwenye huduma za kifedha kupitia makampuni ya simu ni Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zinazoongoza katika bara la Afrika

Dkt. Ndugulile

Ameongeza kuwa, kumekuwa na mafanikio makubwa kama nchi kwa kufikisha huduma za kifedha kwa wananchi wengi nchini kupitia mitandao ya simu ambapo zaidi ya watu milioni 32 wanatumia huduma hiyo na kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 15 hadi trilioni 20 zinazunguka kwenye mitandao hiyo kwa mwezi.



Tukiwa na mawasiliano ya ndani kwa nchi za SADC yatapunguza gharama za mawasiliano na kuwezesha kufanyika kwa shughuli za kiuchumi na maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwezesha kutuma na kupokea fedha ndani ya nchi za SADC kupitia makampuni ya simu

Dkt. Ndugulile

Dkt. Ndugulile amesema kuwa Serikali inaendelea na mikakati yake ya kuwezesha upatikanani wa vifaa vinavyotumia intaneti kwa gharama nafuu kwa kujenga kiwanda cha kuunganisha simu janja na kukaribisha wawekezaji wengine kujenga viwanda vya kutengeneza na kuunganisha simu janja nchini. Amesema kuwa kwa kufanya hivyo itawarahisishia wananchi wenye kipato kidogo kuweza kununua simu janja yenye uwezo wa kufanya matumizi mbalimbali ya intaneti.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Kindamba amesema kuwa ndani ya miezi 12 watahakikisha umoja wa SATA unakuwa na Regional Integration hub itakayosaidia kurahisisha na kupunguza gharama za huduma za mawasiliano baina ya nchi hizo na kuahidi kuwa watakaa na mamlaka za usimamizi wa fedha kuangalia namna ya kuhamisha fedha kutoka nchi moja kwenda nyingine za umoja huo kupitia makampuni ya simu

Ameongeza kuwa, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao TTCL ndio msimamizi wa Mkongo huo na hivi karibuni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile atazindua Kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unakaounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

 

 

Post a Comment

0 Comments