📌MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri Kilimo
Mhe. Hussein Bashe amekutana na Wadau wa
Sekta ndogo ya zao la chai kutoka Serikalini na Sekta binafsi ili kupata
mrejesho wa hatua za uanzishwaji wa mnada wa zao la chai nchini na kusisitiza
ulazima wa kuanza kwa mnada huo na manufaa yake kwa Wakulima na Taifa kwa
ujumla.
Naibu Waziri Bashe
amesema, lengo la mkutano huo uliofanyika leo jijini Dodoma ni kujadiliana namna ya kuongeza uharaka wa juhudi za uanzishwaji wa mnada wa chai ambao
utaenda sambamba na uanzishwaji wa maabara pamoja na maghala ya kuhifadhi chai
hiyo pamoja na ujenzi wa mazingira mazuri ya biashara ya majani ya chai.
Kikao hicho
kimewakutanisha Wadau kutoka Serikalini akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai,
Nicholous Mahuya, Mkurugeni Mkuu wa Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai, Theophord
Ndunguru, Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa za Mazao ya Kilimo (TMX), Godfrey
Malekano.
Wadau wengine wa Sekta
Binafsi ni pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula,
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) Dkt. Emmanuel
Simbua, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya AGRI – CONNECT, Colin Scott na Wadau wengine kutoka Taasisi zinazotoa huduma usafirishaji
wa mizigo katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Naibu Waziri Bashe
amesema, Serikali inafanya juhudi kubwa kuanzisha mnada wa chai nchini, ambapo
haukuwepo kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi kwenye Sekta ndogo ya chai
ambao utakuwa na manufaa na faida nyingi kwa Wakulima wa chai nchini.
Naibu Waziri Bashe
ametoa mfano kuwa usafirishaji wa kontena moja la majani ya chai la urefu wa
futi ishirini kutoka Mufindi kwenda kwenye mnada wa Mombasa nchini Kenya; Gharama
yake ni shilingi milioni sita (6,000,000) wakati kontena hilo hilo, linasafirishwa
kutoka Mufindi kwenda Jijini, Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi milioni
tatu (3,000,000).
Tukipunguza gharama za biashara moja kwa moja na bei kwa Mkulima nayo itapanda. Faida ya pili ya kuwa na mnada nchini ni kuwa tutakuwa na uwezo wa kutawala (Control) bei ya chai sokoni na kuongeza uwazi wa mnyumbuliko wa gharama za uzalishaji wa chai kwa Wakulima wetu
“Tatu, tutakuwa na
uhakika wa ubora wa madaraja ya chai kwenye soko kwa sababu tutakuwa na maabara
yetu; Sasa hivi hatuna uwezo huo kwa kuwa udhibiti wa madaraja ya chai yetu,
unafanywa na Waendeshaji wa minada kwenye nchini nyingine”. Amekaririwa Naibu
Waziri Bashe.
Naibu Waziri Bashe
ameongeza kuwa kwa muda mrefu chai ya Tanzania imekuwa bora na kusisitiza kuwa uanzishwaji
wa maabara ya chai hapa nchini, utaongeza ubora wa chai mara dufu kwa kuwa
itakuwa rahisi kuitambua chai kwa ubora wake kijiografia.
Naye Mwenyekiti wa
Taasisi ya Sekta Binafsi, Angelina Ngalula amesema Sekta Binafsi imejiandaa na
itashirikiana na Serikali katika kujenga mazingira mazuri mazuri ya ufanyaji
biashara ya majani ya chai na kuongeza kuwa TPSF ipo tayari kununua vifaa vya
maabara ya kisasa ya zao la chai pamoja na ujenzi wa majengo maalum kwa ajili
ya maabara hiyo.
0 Comments