📌FAUSTINE GIMU GALAFONI
MKURUGENZI wa
Mashtaka hapa nchini ,Biswalo Mganga ametoa maelekezo kwa vyombo vyote
vya upelelezi nchini kutorejesha fedha kwa watu walioshiriki katika makosa ya
upatu .
Mkurugenzi huyo wa
Mashtaka amebainisha hayo Machi,15,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza
na Waandishi wa Habari kuhusu kuibuka upya kwa biashara haramu ya
upatu hapa nchini kwa kupitia mitandao .
“Kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika
ibara ya 59B ya katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 na vifungu vya 8 na 9[1][c] vya sheria ya usimamizi wa mashtaka
[Sura ya 430 Marejeo ya 2019],ninatoa maelekezo
kwa vyombo vyote vya upelelezi kutorejesha fedha kwa watu
walioshiriki katika makosa ya upatu,amesema.
Mkurugenzi huyo wa
mashtaka amesema siku za hivi karibuni ,kumekuwa na wimbi kubwa la
mipango ya udanganyifu inayodai kutoa fursa za uwekezaji na biashara kwa
wananchi ambayo imekuwa ikiwaaminisha kupata faida
kubwa kwa kipindi kifupi na wanaojiunga wanahamasishwa kushawishi
watu wengine kujiunga na mipango hiyo na waendeshaji wa mipango
hiyo wamekuwa na desturi ya kutumia watu wenye ushawishi kwenye
jamii kama vile viongozi wa dini ili kujenga imani na kuvutia washiriki wapya.
“Mipango hii inafanyika pasipo kupata idhini
ama vibali kutoka katika mamlaka za serikali na hawana
ofisi rasmi zinazotambulika katika uendeshaji wa shughuli zao
,hivyo napenda kuchukua fursa hii kuutahadharisha umma juu ya mipango hiyo
danganyifu inayopotosha umma kuwa ni uwekezaji halali wakati ni
biashara haramu ya upatu na mipango hii imekuwa ikitangazwa kupitia mikutano
ya uhamasishaji na mitandao ya kijamii,amesema.
Hivyo,Mganga amesema
hiyo ni biashara haramu ya upatu [Pyramid schemes] na ni kosa la jinai chini ya
vifungu vya 171A,171B,171C vya sheria ya kanuni ya Adhabu ,Sura ya
16] na vinakiuka masharti ya sheria ya Benki na taasisi za kifedha
Na.5 ya mwaka 2006 inayokataza mtu yeyote kupokea miamala ya
kifedha toka kwenye umma bila leseni.
Ikumbukwe kuwa ,kujihusisha na mipango hii ni kosa la jinai sio tu kwa anayehamasisha na kupokea fedha ,bali hata kwa wanaotoa fedha hizo ,hivyo wanaoshiriki katika biashara hizo wapo katika hatari kupoteza fedha zao pamoja na kushtakiwa mahakamani kwa kosa la kushiriki biashara haramu ya upatu,amesema.
Mkurugenzi huyo wa
mashtaka ameendelea kufafanua kuwa mipango hiyo ni ya kilaghai na imewahi
kujitokeza siku za nyuma na kusababisha wananchi wengi
kupoteza fedha zao huku akizitaja kampuni zilizoshiriki
katika udanganyifu wa michezo ya upatu ni pamoja na Rifaro
Africa,IMS,D9,Miradi ya kuku kupitia kampuni ya Mr Kuku na
Development Entreneurship Initiative [DECI].
Amebainisha kuwa kwa
sasa mipango hiyo imeibuka kwa sura mpya kama biashara ya
kimtandao na wananchi wanaalikwa kushiriki na kuwashawishi
wengine kujiunga huku akitolea mfano kampuni ya QNET LIMITED.
“Kampuni hii imefunguliwa nchini Hong
Kong na inajihusisha na biashara ya kuuza bidhaa kwa njia ya
mtandao kupitia anwani yao ya WWW.qnet.net imeweka
masharti mawili kwa anayetaka kujiunga na biashara yao ,kwanza wanataka
kuhudhuria mafunzo ya kumwezesha kuwa mwanachama na pili
mwanachama mpya analazimika kushawishi wengine kujiunga na kununua
bidhaa za kampuni hiyo na anayefanikiwa kushawishi wengine kujiunga
anapewa ahadi ya kupata kamisheni ,amefafanua.
Mkurugenzi huyo wa
mashtaka ameendelea kusema kuwa mnamo tarehe 1,Februari ,2021 kampuni hiyo
ilimwandikia barua katibu mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara na kumpatia
nakala mkurugenzi wa mashtaka huku ikimtaka kuchukua hatua za kulinda mazingira
ya kampuni hiyo kufanya biashara nchini ili kuipa
hakikisho la kutokubughudhiwa na vyombo ama mamlaka za
serikali ambapo amesema hilo sio moja ya jukumu la mkurugenzi wa
mashtaka.
“Biashara inayofanywa na kampuni hii ni
biashara haramu ya upatu ambayo ni kosa la jinai ,kwa muktadha huo siwezi
kulinda wahalifu ama kuweka mazingira mazuri ya wahalifu kuendelea
kutenda vitendo vya kihalifu ,kwa msingi huo nimeagiza vyombo vya vya upelelezi
kufanya upelelezi wa kina ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwahoji wote
wanaohusika na nimebaini baadhi ya taasisi za serikali zimekuwa zikirejesha
fedha kwa baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni
wahanga wa uhalifu huo wa upatu “amesema.
0 Comments