Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema ili kukabiliana na kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa zao la chai nchini wizara yake itawekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uzalishaji wa miche bora ili zao la chai lilimwe kwenye maeneo mengi nchini
Amesema wizara ya kilimo
itahakikisha inatumia wataalaam wake wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na taasisi
za fedha kupata mitaji itakayowekezwa kwenye kujenga miundombinu muhimu ya
umwagiliaji ili zao la chai ambalo linastawi kwenye wilaya zaidi ya kumi na
mbili nchini lilimwe na kuvunwa mwaka mzima.
“Tutafuta fedha toka kwa
wadau wa taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) ili
tujenge miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima wadogo wa chai
hatua itakayohakikisha tunaongeza uzalishaji wa majani mabichi ya chai mwaka
mzima badala ya kutegemea mvua” alisema
Prof. Mkenda.
Waziri wa Kilimo ametoa kauli
hiyo jana (11.03.2021)wakati alipotembelea mashamba ya wakulima wadogo wa chai
kijiji cha Lwanga wilaya ya Njombe wanaoratibiwa na kampuni ya huduma kwa
wakulima Wadogo Njombe (NOSC).
Waziri Mkenda aliogeza kusema
ili kukuza uzalishaji wa zao la chai suala la kutumia teknolojia ya umwagiliaji
na matumizi ya miche bora ni muhimu na kuwa wizara itatafuta wadau kusaidia
wakulima wadogo kumwagilia mashamba yao .
Prof. Mkenda aliwasihi
wanachama wa NOSC kupanua mashamba yao kwani wana uhakika wa soko kwenye
kiwanda cha kampuni ya Unilever (UTT) inayonunua majani mabichi ya chai ya
wakulima hao.
Aidha, Waziri huyo wa kilimo
aliagiza bodi ya chai na Taasisi utafiti wa zao la chai (TRIT) kuzalisha miche
bora ya chai na kuigawa kwa wakulima ili wapanue mashamba mapya na kuziba
mapengo kwenye mashamba ya zamani.
Akitoa taarifa ya utendaji
kazi wa kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe (Njombe Outgrowers Services
Company –NOSC) Meneja Mkuu wake John Mhagama alisema wamefanikiwa kuanzisha
mashamba mapya ya chai hekta 1,345 kati ya kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019.
Aliongeza kusema katika mwaka
2020/2021 wamepanda hekta 275 hivyo kupelekea kufikia jumla ya hekta 1,620 za
mashamba mapya ya chai.
Kuhusu kiwango cha uzalishaji
chai Mhagama alisema wakulima wadogo wameongeza uzalishaji toka kilo 3,364 za
majani mabichi kwa hekta hadi kilo 5,977
na sasa lengo ni kufikia wastani wa kilo 11,250 endapo miundombinu ya
umwagiliaji ikikamilika.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi
Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakulima Wadogo wa Chai Phillemon Luhanjo
alishukuru serikali kupitia waziri wa kilimo kwa kuwasaidia wakulima kupata
huduma za ugani hatua inayokuza ubora wa chai.
“Sisi wakulima wakulima
tunafurahi kuiona serikali ikifuatilia utendaji kazi wetu na kututia moyo
tuendelee kuhudumia mashamba yetu ya chai .Tutaongeza mashamba mapya ili lengo
la nchi lifikiwe “ alisema Mzee Luhanjo ambaye pia ni mkulima wa chai.
Kwa mwaka uzalishaji wa
majani mabichi ya chai kwa mujibu wa takwimu za bodi ya chai umefikia tani
32,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima kwenye wilaya zote 12 zinazolima zao hilo
nchini.
Ziara hii ya Waziri Mkenda
kwa wakulima wadogo wa chai inafuatia kikao cha wadau wa zao la chai
kilichofanyika mkoani Njombe juzi chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa ambaye aliagiza Wizara kuwa na utaratibu wa kuwatembelea wadau kujua
namna ya kutatua kero .
Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Kilimo
NJOMBE
11.03.2021
0 Comments