WAZIRI wa Kilimo Profesa
Adolf Mkenda amesema ili kukabiliana na kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa
zao la chai nchini wizara yake itawekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uzalishaji
wa miche bora ili zao la chai lilimwe kwenye maeneo mengi nchini.
Amesema wizara ya kilimo
itahakikisha inatumia wataalaam wake wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na taasisi
za fedha kupata mitaji itakayowekezwa kwenye kujenga miundombinu muhimu ya umwagiliaji
ili zao la chai ambalo linastawi kwenye wilaya zaidi ya kumi na mbili nchini
lilimwe na kuvunwa mwaka mzima.
“Tutafuta fedha toka kwa
wadau wa taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) ili
tujenge miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima wadogo wa chai
hatua itakayohakikisha tunaongeza uzalishaji wa majani mabichi ya chai mwaka
mzima badala ya kutegemea mvua” alisema
Prof. Mkenda.
Waziri wa Kilimo ametoa
kauli hiyo jana (11.03.2021)wakati alipotembelea mashamba ya wakulima wadogo wa
chai kijiji cha Lwanga wilaya ya Njombe wanaoratibiwa na kampuni ya huduma kwa
wakulima Wadogo Njombe (NOSC).
Waziri Mkenda aliogeza
kusema ili kukuza uzalishaji wa zao la chai suala la kutumia teknolojia ya
umwagiliaji na matumizi ya miche bora ni muhimu na kuwa wizara itatafuta wadau
kusaidia wakulima wadogo kumwagilia mashamba yao .
Prof. Mkenda aliwasihi
wanachama wa NOSC kupanua mashamba yao kwani wana uhakika wa soko kwenye
kiwanda cha kampuni ya Unilever (UTT) inayonunua majani mabichi ya chai ya
wakulima hao.
Aidha, Waziri huyo wa
kilimo aliagiza bodi ya chai na Taasisi utafiti wa zao la chai (TRIT) kuzalisha
miche bora ya chai na kuigawa kwa wakulima ili wapanue mashamba mapya na kuziba
mapengo kwenye mashamba ya zamani.
Akitoa taarifa ya utendaji
kazi wa kampuni ya kuhudumia wakulima wadogo Njombe (Njombe Outgrowers Services
Company –NOSC) Meneja Mkuu wake John Mhagama alisema wamefanikiwa kuanzisha
mashamba mapya ya chai hekta 1,345 kati ya kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019.
Aliongeza kusema katika
mwaka 2020/2021 wamepanda hekta 275 hivyo kupelekea kufikia jumla ya hekta
1,620 za mashamba mapya ya chai.
Kuhusu kiwango cha
uzalishaji chai Mhagama alisema wakulima wadogo wameongeza uzalishaji toka kilo
3,364 za majani mabichi kwa hekta hadi
kilo 5,977 na sasa lengo ni kufikia wastani wa kilo 11,250 endapo miundombinu
ya umwagiliaji ikikamilika.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi
Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakulima Wadogo wa Chai Phillemon Luhanjo
alishukuru serikali kupitia waziri wa kilimo kwa kuwasaidia wakulima kupata
huduma za ugani hatua inayokuza ubora wa chai.
“Sisi wakulima wakulima
tunafurahi kuiona serikali ikifuatilia utendaji kazi wetu na kututia moyo
tuendelee kuhudumia mashamba yetu ya chai .Tutaongeza mashamba mapya ili lengo
la nchi lifikiwe “ alisema Mzee Luhanjo ambaye pia ni mkulima wa chai.
Kwa mwaka uzalishaji wa
majani mabichi ya chai kwa mujibu wa takwimu za bodi ya chai umefikia tani
32,000 kwa mwaka kutoka kwa wakulima kwenye wilaya zote 12 zinazolima zao hilo nchini.
Ziara hii ya Waziri Mkenda
kwa wakulima wadogo wa chai inafuatia kikao cha wadau wa zao la chai
kilichofanyika mkoani Njombe juzi chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa ambaye aliagiza Wizara kuwa na utaratibu wa kuwatembelea wadau kujua
namna ya kutatua kero .
Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Kilimo
NJOMBE
11.03.2021
0 Comments