KAMATI ya Kudumu ya
Bunge ya Kilimo ,Mifugo na Maji imepongeza jitihada za wizara ya kilimo
kuzalisha mbegu bora za mazao ya kilimo kupitia Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA)
Hayo yameelezwa leo
Morogoro (15.03.2021) na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Christine Ishengoma
alipoongoza wajumbe kukagua utendaji kazi wa Wakala wa Mbegu nchini (ASA)
pamoja na ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI).
Tunapongeza wakala wa mbegu ASA kwa kushika nafasi ya tano kati ya makampuni 42 yanayozalisha mbegu ambapo kwa mwaka 2019/20 ilizalisha tani 1,750 za mazao mbalimbali
Dkt.Ishengoma.
Naye Mtendaji Mkuu wa
ASA Dkt. Sophia Kashenge akiwasilisha taarifa kwa kamati ya kudumu ya Bunge
alisema kwa kushirikiana na makampuni manane wamefanikiwa kuzalisha mbegu
kwenye mashamba ya serikali toka tani 3,450 mwaka 2016/17 hadi tani 5,634 mwaka
2019/20.
Dkt.Kashenge aliongeza
kusema katika kipindi cha miaka minne iliyopita wakala umefanikiwakuzalisha
miche 342,000 ya michikichi ambapo miche 10,200 tayari imegawiwa bure kwa
wakulima kwenye wilaya nne za Mkoa wa Kigoma kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Waziri
wa Kilimo Prof.Adolf Mkenda alisema ili kuhakikisha nchi inafikia utoshelevu wa
uzalishaji mbegu za mazao ya kilimo atazikutanisha taasisi za ASA,TOSCI na TARI
ili kujadili na kuweka mkakati wa pamoja wa kitaalam kuwezesha upatikanaji wa
mbegu bora nyingi.
Prof. Mkenda
aliwashukuru wabunge kwa kutembelea taasisi hizo zenye kazi kubwa ya
kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa uzalishaji mbegu na kuwa katika bajeti
ijayo 2021/22 wizara itaomba Bunge kupitisha makadirio ya bajeti ili sekta ya
mbegu ipate fedha za kutosha.
Takwimu zinaonesha
katika kipindi cha miaka minne upatikanaji wa mbegu umeongezeka kutoka tani
36,614 mwaka 2015/16 hadi tani 76,725 mwaka 2019/20 huku uzalishaji wa ndani wa
mbegu bora umeongezeka kutoka tani 20,604 mwaka 2015/16 hadi tani 69,173 mwaka
2019/20.
(Habari na picha na
Wizara ya Kilimo)
0 Comments