FAO KUWAINUA WAVUVI WADOGO KIUCHUMI.

 





📌JASMINE SHAMWEPU.

SEKTA ya uvuvi inachangia asilimia 1.7 katika ukuaji wa uchumi wa nchi. Hata hivyo, licha ya asilimia kubwa ya nchi yetu kuwa na sehemu kubwa iliyozungukwa na maziwa, mito na bahari, lakini mchango katika sekta ya uvuvi bado haujaleta mafanikio ya kutosha ikilinganishwa na rasilimali zilizopo.

 Hii inatokana na utumiaji wa zana duni katika uvuvi Pamoja na njia za asili ambazo zimechangia uharibifu wa mazingira na umaskini.

Kutokana na sababu hizo na nyinginezo, sekta hii imekosa hamasa na kipaumbele na kushindwa kutoa mchango katika maendeleo ya jamii.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wake inafanya mapinduzi na mabadiliko katika sekta hii. Mwandishi wetu aliyetembelea mradi mpya wa uvuvi kwa nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (FISH4ACP) katika Ziwa Tanganyika anafafanua katika makala hii.

Tofauti kubwa ya shughuli za uvuvi inabainishwa kwa kutazama zana za uvuvi za asili na zana za kisasa, kumlinganisha mvuvi wa kale na mvuvi wa kisasa, kuangalia ubora na wingi wa mazao ya ziwani yaani samaki na dagaa wanaozalishwa na vitu vingine vingi kama hali duni ya maisha ya familia ya mvuvi na mfanyabiashara mwingine wa samaki kando ya Ziwa Tanganyika na maeneo mengine ya nchi.

Anna Onesmo ni mfanyabiashara wa dagaa katika soko la Kibirizi mkoani Kigoma, anayejaribu kupambana na hali duni ya biashara ya dagaa bila msaada wa kupata fursa za kukuza mtaji wake kwa njia ya mikopo yenye riba nafuu wala mafunzo endelevu ili kuboresha bidhaa yake. 

Hata hivyo, anasema uanikaji mzuri wa dagaa umemsaidia kuondoa mchanga na sasa anaweza kupata wanunuzi wengi ambao hawalalamiki kama zamani. Licha ya kupata soko la  ndani na nje bado anakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu na mazingira mabovu ya soko hasa nyakati za mvua ambapo soko linajaa maji machafu na wafanyabiashara wenzake wanakosa sehemu salama za kukaa na kufanya biashara zao.

“Tulikuwa tunaanika na kukausha dagaa chini kwenye mchanga na kupunguza ubora wa bidhaa kwa wanunuzi kutoka nje, lakini kwa sasa hakuna mchanga kwenye dagaa na wanunuzi wanakuja kwa wingi,” anaeleza Anna, huku akiomba vyombo vyenye dhamana ya kusimamia  maendeleo ya sekta hiyo, kuwajengea miundombinu ya kisasa ili kuendeleza biashara yake.

Kuhusu tozo za kodi anasema zipo juu na kuiomba Serikali kuangalia njia bora ya kupunguza kodi, kwani wafanyabiashara wadogo ambao ni wanawake wanalazimika kutegemea wafanyabiashara wakubwa kusafirisha ambao wanafidia gharama zao kwa kuwabana wafanyabiashara wadogo kwa kuwauzia kwa bei ya juu.

“Ikiwezekana tutafutiwe ndege ya kwenda nje moja kwa moja kama wenzetu wa Mwanza wanaofaidika kwa usafirishaji wa anga kwenda soko la Ulaya kwenye masoko ya kimataifa,” anasema Anna Onesmo.

Anaongeza, “matarajio ni kufikia ubora wa dagaa na kupata soko la ndani na nje licha ya kuwepo kwa changamoto za mtaji na gharama kubwa za uendeshaji.”

Mkazi mwingine wa Kibirizi na mwenyekiti wa vipe yaani zana za uvuvi, Alhaj Amiri Hamim, anasema zana duni za uvuvi kama kikwazo cha kukuza maaendeleo ya sekta ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika huku akitupia kilio chake kwa serikali kutaka wavuvi wawezeshwe  kwa kuwekeza mtaji kwa njia ya mikopo nafuu kama ilivyokuwa inafanya zamani kupitia benki ya CRDB.

“Kwa kweli kukosa kuungwa mkono na serikali mbali na changamoto za ushuru mwingi na kodi kubwa kunawaweka njia panda wadau wa sekta hiyo kwa  kuwatofautisha na wakulima waliopunguziwa orodha ndefu ya ushuru wa mazao na pembejeo,” anasema.

Ameongeza kusema, ili kukabili changamoto hizo wavuvi wanahitaji zana bora na za kisasa za uvuvi na kuomba Serikali kuwatambua wavuvi wadogo kwa kuwajengea mazingira rafiki ya kuendesha shughuli za uvuvi na kuwapa mikopo yenye riba nafuu.

Wakati huo huo, anakiri kwa sasa watu wanakula dagaa bora bila mchanga kama ilivyokuwa zamani na kwamba baada ya kupata mafunzo chini ya mradi wa serikali uliopita, uzalishaji na uhifadhi wa dagaa umeboreshwa na kuwezesha soko la dagaa kupanuka.

“Ombi letu kubwa kwa Serikali ni kurudisha mikopo ya zana bora za uvuvi na kwamba mradi wa awali uliofungwa zamani ulisababisha wavuvi kukosa vitendea kazi, mafunzo, usimamizi endelevu na zana za kisasa za uvuvi.

Naye Mwanaidi Ramadhani mkazi wa Wilaya ya Uvinza, anasema wafanyabiashara wadogo hawana mtambo wa barafu wa kuhifadhi dagaa na kwamba analazimika kutupa dagaa au kufanya chakula cha mifugo kwa sababu wanabadilika rangi na kutoa harufu hivyo kupata hasara.

Akizungumzia changamoto hiyo hiyo ya kukosa jokofu la kuhifadhi dagaa, Mariam Shaban ambaye pia ni muuza dagaa wa mafungu anasema hofu yake kubwa ni pindi mvua inaonyesha kwa sababu anashindwa kuhifadhi bidhaa yake hivyo kutumia barafu ambayo kwa uhalisia haitoshelezi mahitaji yake.

Katika kujaribu kutatua baadhi ya changamoto za wavuvi, serikali imeanza kuwekeza katika mradi mkubwa kwa kushirikiana na wabia wake wa maaendeleo ikiwemo Jumuiya ya nchi za Ulaya na Serikali ya Ujerumani. 

Mradi huo unalenga kuleta mabadiliko makubwa kwa wavuvi na wadau wa sekta hiyo.

Mtaalam wa Kitaifa wa uvuvi kutoka Shirika la Chakula na Kilimo (FAO, Tanzania), Hashim Muumin anazungumzia mradi huo unaolenga kuangalia changamoto za uvuvi wa samaki katika Ziwa Tanganyika kuanzia mnyororo wa thamani kutoka hatua za uvuvi wa nyavu hadi kwenye sahani.

“Ni mradi utakaoangalia kwa undani na kujibu maswali kuhusu sababu za kushindwa kufunguka kwa sekta ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika ikilinganishwa na uvuvi katika Ziwa Victoria,” anafafanua.

Mradi wa FISH4ACP ulioanza Oktoba 2020 – utadumu kwa kipindi cha miaka 5 kwa kuangalia zaidi changamoto na fursa kwenye uzalishaji wa samaki wanaopendwa katika ziwa hilo hasa aina ya migebuka na dagaa wa Kigoma.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya fedha za kigeni Euro milioni 3 kwa kuboresha uvuvi wa samaki aina tata wakiwemo dagaa na migebuka katika Ziwa Tanganyika  linalokadiriwa kuwa na wavuvi wadogo 27, 000 na boti 12,000.

Kwa mujibu wa taarifa za FAO Ziwa Taanganyika lina aina 350 ya samaki wakiwemo samaki wa mapambo takriban aina 250 ambao bado uzalishaji wake haujapewa kipaumbele licha ya kuwa na thamani kubwa.

Inakadiriwa mojawapo wa aina hizo za samaki wanaweza kuuzwa kwa dola za Kimarekani 200 kwa kila mmoja.

Katika utekelezaji wa mradi huo, mwaka wa kwanza unatarajiwa kutumika kufanya uchambuzi wa kina kujua na kuuangalia changamoto kutoka kwa wadau wa sekta ya uvuvi, wakiwemo wavuvi wenyewe, wasimamizi wa sekta ya wavuvi, wachakataji samaki wakubwa na dagaa na wote walioko kwenye mnyororo wa thamani wakiwemo wasafirishaji masafa mafupi na marefu.

“Machi mwaka huu ni kukusanya taarifaa za wadau – changamoto na fursa na kuziangalia kwa undani kwa kuuliza maswali ambayo yatafanyiwa kazi katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaaji wa mradi huo,” anafafanua Hashim Muumin mtaalam kutoka FAO.

“Baada ya miaka mitano tunakwenda kupindua na kubadilisha maisha ya wavuvi kwa uzoefu wetu mkubwa na wa muda mrefu ambapo wavuvi wa Ziwa Tanganyika tunawasihi waupokee mradi huu kwa kujibu maswali kwa makini wakieleza wanavyoona.  Wasibabaishe majibu kwani tunataka watwambie hali halisi,” anasema na kuongeza, “Ukisema uongo na mipango itakuwa ya uongo kwa hiyo waseme ili tuweze kuwasaidia.”

Uchunguzi wa awali hadi sasa unabainisha kuwa changamoto kubwa za uvuvi ni kati ya asilimia 40 hadi 70 ya samaki wakubwa na dagaa hupotea kutokana na miundombinu mibovu na zana hafifu za uzalishaji, kuhifadhi na kuchakata mazao hayo na asilimia 30 ndio hufika kwa mlaji.

Dr Ishmael Kimirei mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI), anakiri kuwepo kwa changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, na mabadiliko ya mazingira na baadhi ya wadau wanaodai aina ya mitego inayotumika kuvua samaki inasababisha uharibifu mkubwa.

“Sisi katika hatua za uchambuzi tunataka kujua nini kifanyike kuboresha sekta hiyo na hatimaye kwa pamoja kutimiza lengo kuu la kuibua fursa za uvuvi katika mnyororo wa thamani kuanzia hatua ya mwanzo hadi kwa mlaji na kuboresha sekta nzima ya uvuvi kwa watu wanaozunguka Ziwa Tanganyika.”  

Akiwa msimamizi mkuu wa mradi unaokwenda kufungua fursa  za uvuvi katika Ziwa Tanganyika, kwa Tanzania mradi huo utagharimiwa na Serikali ya Ujerumani  kwa ushirikiano na Jumuiya ya Ulaya EU- kwa gharama ya EURO 40 milioni ambapo utahusisha nchi 12 za Afrika ambazo ni Gambia, Nigeria, Tanzania, Zimbabwe na Zambia na nchi za Caribbean ni Guinea na Jamhuri ya Dominica ambapo Tanzania inapata fursa ya kuwekeza katika uvuvi Ziwa Tanganyika, chini ya mradi unatekelezwa na Shirikka la chakula  na kilimo (FAO) kwa ushirikiano na TAFIRI –Taasisi ya utafiti wa samaki chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Kwa mujibu wa Dr Kimirei awamu ya kwanza, ni uchambuzi na kuja na mikakati ya kufungua fursa za uvuvi ndipo kuanza kutatua matatizo na changamoto zinazokwamisha maendeleo ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika mfano masoko, zana za uvuvi zikiwemo nyavu, uchakataji samaki na matatizo mengine ambayo yataibuka baada ya utafiti na lengo kuu ni kuifanya sekta hiyo kuwa rasmi na yenye  mchango katika pato la mwananchi na  Taifa kwa ujumla.

 Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments