Wanaushirika kutoka vyama vya ushirika maeneo mbalimbali Tanzania wakifuatilia mada mbalimbali zinazotolewa katika kongamano la kwanza la tafiti za ushirika lenye kaulimbiu isemayo “Utafiti kwa maendeleo ya ushirika”lililoanza Machi,16,2021 na kuhitimishwa leo Machi,18,2021.
📌FAUSTINE GIMU GALAFONI.
Katika utafiti uliofanyika mwezi MEI,2020 kwa kushirikiana na wanafunzi wa mwaka wa pili wa sheria za ushirika wa chuo kikuu cha Ushirika Moshi [MOCU] ulibaini kutokuwa na uelewa kwa viongozi wa vyama vya ushirika mbalimbali kuhusu sheria za ushirika ikiwa ni pamoja na masharti ya vyama vyao.
Akitoa wasilisho la utafiti juu ya uelewa wa viongozi wa vyama vya ushirika kuhusu sheria ,maadili na misingi ya ushirika katika kongamano la kwanza la tafiti za ushirika lenye kaulimbiu isemayo “Utafiti kwa maendeleo ya ushirika”Mhadhiri mwandamizi kutoka chuo kikuu cha Ushirika Moshi[MOCU],Dkt.Audax Peter Rutabanzibwa alisema takriban asilimia 96% ya viongozi wa vyama vya ushirika vilivyofanyiwa utafiti hawana uelewa kuhusu sheria na kanuni za ushirika.
Dkt. Rutabanzibwa alisema ni asilimia 10% tu ya viongozi wa vyama vya ushirika vilivyofanyiwa utafiti wana uelewa kuhusu masharti ya vyama vyao .
Sababu zilizotolewa na viongozi kutokuwa na uelewa na masharti,kanuni na sheria za vyama vyao ni pamoja na kanuni ,taratibu na sheria hizo kuandikwa kwa lugha ya kisheria ambayo ni vigumu sana kwa watu wa kawaida kuelewa sheria hizo ambao wengi wao ndio wanachama .
Dkt. Rutabanzibwa alisema kuna madhara makubwa kwa viongozi kutokuelewa masharti ya vyama vyao katika maendeleo ya ushirika nchini ambapo utafiti unapendekeza kuwa elimu ya sheria na kanuni za ushirika iwe inatolewa kwa viongozi wa vyama vya ushirika mara tu viongozi hao wanapochaguliwa na ni muhimu sheria na kanuni hizo zitafsiriwe katika lugha rahisi ili wanachama na viongozi waweze kuzielewa.
Aidha.Dkt. Rutabanzibwa alisema utafiti unapendekeza kuwa ili kuepuka vyama vya ushirika kuongozwa na viongozi wasiotanguliza maslahi ya vyama ,kigezo au kipimo cha uelewa na kuwa tayari kutekeleza masharti ya chama kiwe ni mojawapo ya sifa muhimu za mwanachama wa chama cha ushirika kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama.
Utafiti huo ulihusisha kwa viongozi wa vyama vya ushirika 75 kati ya vyama 100 vilivyotembelewa ambapo ilijumuisha vyama vikuu 5 ,vyama vya msingi [AMCOS na SACCOS 50 na vyama vya ushirika aina nyingine 4 ambapo taarifa za vyama 25 hazikuthibishwa na mameneja wa vyama wala maafisa ushirika wa wilaya hivyo havikuhusishwa katika uchambuzi wa utafiti.
Dkt. Rutabanzibwa aliainisha mapendekezo manne katika utafiti huo kuwa ni pamoja na elimu ya sheria na kanuni za ushirika kutolewa kwa viongozi mara tu wanapochaguliwa,Sheria na kanuni zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili,kigezo cha kuchagua viongozi wanaotanguliza maslahi ya chama na wanachama kuwezeshwa kutafsiri matendo na masharti ya vyama vyao.
Wakati huohuo Vyama vya Ushirika hapa nchini vimetakiwa kuanzisha mifuko ya utafiti hali itakayosaidia kutatua changamoto za wakulima kwa ufasaha.
Hayo yalibainishwa Machi,16,2021 jijini Dodoma na Naibu katibu mkuu wizara ya kilimo Prof.Siza Tumbo wakati wa ufunguzi wa kongamano la kwanza la tafiti za ushirika ambalo limeandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini[TCDC].
Prof.Tumbo alisema fedha za kutegemea wadau kutoka nje zimekuwa na masharti magumu hivyo ili kuondokana na vikwazo ni vyema kuanzisha mifuko ya utafiti.
Aidha,Prof.Tumbo alisema licha ya kuwezesha tafiti nyingi nchini,bado tafiti hizo hazina majibu ya kero za wananchi hivyo kuwataka watafiti kutumia muda mwingi kufanya tafiti za masuala ya masoko huku pia akionya kwa baadhi ya wana Ushirika wanaoingia kwenye vyama hivyo kwa lengo la kujitajirisha .
Naye Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Dkt.Benson Ndiege alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni fursa kwa kuwa limewakutanisha wadau wa maendeleo ya ushirika kukutana na wanachama ,viongozi watendaji hivyo kuwa na matumaini zaidi katika kuleta matokeo ya tafiti mbalimbali za ushirika zilizowahi kufanyika na mapendekezo yake na kupata utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Sambamba na lengo kuu,Mrajis huyo aliainisha matarajio mengine kwenye kongamano hilo ni kupata mambo yatakayoibuliwa na washiriki ikiwa ni pamoja na vipaumbele vitakavyoainishwa vitafanyiwa utafiti ambapo maamuzi yake yatakuwa shirikishi ili kurahisisha utekelezaji.
Kwa upande wake Meneja mkuu chama cha ushirika cha mradi wa pamoja zao la tumbaku[TCJE]Bakari Hussein alisema bado suala la elimu lipo chini kwa wana ushirika hivyo inahitajika zaidi na si kwa viongozi pekee.
Kongamano la kwanza la tafiti za ushirika linafanyika kwa siku tatu jijini Dodoma kuanzia Machi 16 -18/2021 huku kaulimbiu ikisema”Tafiti kwa maendeleo ya ushirika.
MWISHO.
0 Comments