Mkufunzi wa maswala ya habari Tanzania Dkt,Ananilea Nkya amesema ili vyombo vya habari viweze kuchangia maendeleo ya Nchi lazima wazingatie habari zinazogusa maendeleo ya wananchi moja kwa moja.
Ameyasema hayo wakati akiendelea na mafunzo kwa waanidishi wa habari vijana Zanzibar yalioratibiwa na TAMWA,ZAFELA,PEGAO chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway Nchini, yaliofanyika katika ukumbi wa Malaria mjini hapa.
Amesema habari zinazogusa wananchi ni zile ambazo zinagusa maisha ya wananchi ikiwemo kijamii na kiuchumi na ndio aina ya habari ambazo zikifanyw ani wazi kuwa zitaleta tija kwa Taifa.
Ameeleza kuwa hivi sasa wimbi kubwa la waandishi wa habari visiwani wamesahau wajibu wao na kufanya kazi hio kimazoea jambo ambalo inaonakana wazi kuwa kuna idadi kubwa ya vyanzo vya habari na habari bado zinashindwa kuandikwa wala kuripotiwa.
Mkufunzi huyo aliwataka waandishi wa habari vijana Zanzibar kuondokana na habari zinazoishia kiongozi kasema nini au kafanya nini badala yake wanatakiwa kwenda mbali zaidi ikiwa ni pamoja na kuripoti alichokitekeleza kiongozi kwenye jamii yake na matukio gani yaliopatikana.
Akiendelea kufafanua zaidi alisema ili iweze kuwa bora ni lazima waandishi wa habari wafike eneo husika na kujiridhisha mafanikio ama taarifa zao wanazotaka kuripoti zina uhakika kwa kiasia gani.
Sambamba na hilo aliwataka waandishi hao visiwani hapa wakati wa kuripoti habari za demokrasia na uongozi kwa wanawake wahakikishe wanavikifikia vyanzo vyote vya haabari ikiwemo wananchi wanawake na wanaume pamoja na viongozi husika kwa lengo la kupaza sauti za kila mmoja.
Akitaja miongoni ma faida ya uandishi wa ina hii alisema ni kuleta uwajibikaji kwa viongozi katika ngazi mbali mbali pamoja na matumizi mazuri ya fedha za umma na kuongeza kasi ya kujituma kwa wananchi.
‘’Unaweza kuona uandishi huu ni mgumu zaidi kwa kuwa unastahiki kujituma na kufikiri lakini ndio aina ya uandishi ambao nyinyi vijana mnatakiwa kuwa nao’’aliongeza.
Kwa upande wake mwandishi wa habari mkongwe Zanzibar Salim Said amesema waandishi wa habari wengi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hujisahau wakati wanapotekeleza wajibu wao.
Amesema mwandishi ili waweze kufanya kazi zake inavyopaswa na kupata taarifa muhimu analazimika kutumia akili nyingi zaidi ikiwemo kumuandaa mtu anaetaka kumuhoji.
Ameeleza kuwa mwandishi ni mtu muhimu anaehitaji kujifunza kila leo kwa lengo la kuongeza uelewa na kutafuta mbinu mpya za kukusanya taarifa.
Wakichangia mafunzo hayo baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema kwa muda mrefu wamekua wakikabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuelewa vitu vingi vinavyohusu taaluma hio.
Miongoni mwa waandishi hao ni Miraji Manzi kutoka redio mtegani Makunduchi Unguja alisema kupitia mafunzo hayo yamewajenga upya na anaamini washiriki watafanya makubwa hususani katika taarifa zinazohusu wanawake.
Nae mwandishi kutoka Coconut FM Amina Mchezo alisema waandishi wengi hukosa umakini na huja na maswali yao mkononi jambo ambalo alisema hawawatendei haki vyanzo vyao vya habari.
Amesema kama mwandishi unapokwenda na maswali yako mkononi ni sawa na kuwa hutaweza kumuuliza mengine ambayo hukufaandika awali.
0 Comments