📌DEVOTHA
SONGORWA.
HALMASHAURI Nchini
zimetakiwa kutenga bajeti kupitia mapato ya ndani ili kusaidia shule zenye
mahitaji maalumu na wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki kulingana na
ulemavu wao.
Hayo yamesemwa na
Katibu Mkuu wa Jumuia ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Erasto Sima
alipofanya ziara katika Shule ya Msingi Buigiri ya wasioona ikiwa ni
maadhimisho ya miaka 44 ya CCM tangu kuanzishwa februari 05 mwaka 1977 ambapo
alikabidhi kadi za bima ya afya ya CHF zenye thamani ya shilingi 510,000kwa
wanafunzi 100 na shilingi 100,000 baadhi ya wakazi wa Kata ya Buigiri wasioona
kupata huduma ya matibabu pindi wanapohitaji fedha zilizotolewa na mdau
wa maendeleo.
“Ipo haja ya
halmashauri kujiweka sawa kupitia mapato ya ndani kusaidia shule hizi,wadau na
kila mmoja wetu anayeguswa tufike hapa shuleni tuwasaidie tunatambua wana
mahitaji mengi ndiyo maana Rais,Dk.John Magufuli ameendeleea kutetea
wanyonge na serikali imetoa milioni 80 kujenga bweni la wanafunzi na nimpongeze
mdau huyu aliyewalipia watoto hawa na mimi ninatoa shilingi 500,000
kusaidia matatizo yaliyopo katika shule hii,”alisema Katibu Mkuu huyo.
Pia Katibu Mkuu huyo
aliongoza zoezi la kupanda miti 200 katika shule hiyo akisema hatua hiyo
inawezesha uhifadhi wa mazingira na ishara ya kuenzi viongozi wa serikali
waliosisitiza upandaji miti kukabili changamoto zinazotokana na kukata miti
kiholela huku akiahidi kushirikiana na viongozi wengine kutatua chnagamoto za
shule hiyo.
“Nchi nzima jumuia
inapanda miti na siyo hapa tu Bahi, Kongwa, Kondoa na kwingine wanafanya
hivi maana ni moja ya majukumu tuliyopewa jumuia yetu nitoe wito kwa wananchi
wote kila mtu katika eneo lake apande miti vinginevyo tutakosa mvua, hewa safi
na mabadiliko ya tabianchi wakati yote haya tutayaepuka tukipata miti,”alisema
Sima.
Kwa upande wake Mdau
wa Maendeleo ambaye pia ni Mjasiriamali Elisha Ndulu ameeleza kwamba
kilichomsukuma kufanya hivyo ni upendo alionao kwa watoto na kushiriki baraka
alizojaaliwa na Mungu kuhudumia wenye mahitaji kujiona ni sehemu ya jamii
na wana haki kama watoto wengine wasio na ulemavu.
“Niliguswa sana kama
mzazi na ninachokitoa hakilingani na mahitaji yao namuomna Mungu siku nyingine
nipate zaidi wana mahitaji mengi sana niwaombe wadau wenzangu tuwashike hawa
watoto ni wetu siyo lazima uwe na mamilioni ni kile ulichonacho tuna wajibu
mkubwa kwa hawa watoto,”alieleza Mdau huyo.
Awali akitoa taarifa
Mkuu wa Shule hiyo Samwel Jonathan amesema wanakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo ukosefu wa uzio hali inayohatarisha usalama wa watoto na
mali za shule, uchakavu wa baadhi ya majengo, uhaba wa vitabu vya kiada kwa
wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu akiomba jamii kushiriki kujitolea
kuwasaidia.
“Tunashukuru Serikali
kwa kushirikiana na sisi ila bado tuna mahitaji mengi watoto wengi wanaosoma
hapa wanatoka familia duni ruzuku tunayopokea kila mwezi haikidhi
mahitaji na sasa tunadaiwa na wazabuni zaidi ya milioni 36,miundo mbinu
ya maji siyo rafiki na barabara,upungufu wa vifaa vya bweni magodoro 53,
vyandarua 92,vitanda 11, mashuka 92 na vifaa vya wanafunzi wenye ulemavu
tunaomba anayeguswa atusaidie,”alisema Jonathan.
Aidha akitoa taarifa
ya Chama Cha CCM Katibu Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Chamwino,Ashura Ngade
alieleza kwamba tangu kuzaliwa kwa CCM jumuia ya wazazi imekuwa mstari wa
mbele kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na watoto kupata malezi
stahiki huku akisema jumuia inayo mikakati mbalimbali kujiimarisha
kiuchumi ikiwemo kumiliki ekari 100 kwa ajili ya kupanda korosho.
“Uhai wa jumuia tuna
matawi 242, Kata 36 na wilaya sasa hivi tunafanya maandalizi ya uchaguzi mkuu
wa Chama na jumuia zake kwa mwaka 2020/22, tumejipanga kufanya semina ya
wanachama na viongozi wa jumuia, tutaingiza wanachama wasiopungua 50 kila tawi
na tuna changamoto ya ukosefu fedha na tunawahimiza wazazi kuwa na moyo wa
kujitolea katika shughuli za kuwaletea maendeleo na wilaya yetu ilifanya vizuri
sana katika uchaguzi mkuu wa 2020,”alieleza.Ashura.
Ikumbuke Maadhimisho
ya siku ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hufanyika kila ifikapo
Februari 05 ya kila mwaka tangu kilipoanzishwa mwaka 1977 baada ya kuungana kwa
vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) kilichokuwa kikitawala
Tanzania Bara na Afro-Shirazi Party (ASP) kilichokuwa chama tawala
cha Zanzibar wakati huo.
0 Comments