📌DEVOTHA SONGORWA.
WAJASIRIAMALI na wafanyabiashara nchini
wametakiwa kufuata sheria na taratibu za maonesho ya biashara bila shuruti
kuepuka malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa kwa wananchi ikiwemo
kutapeliwa fedha zao.
Akizungumza jana na mtandao huu Mwanasheria
wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Fikiri Mboya amesema
mamalka hiyo moja ya majukumu yake ni kudhibiti maonesho akisema baadhi ya watu
hupeleka bidhaa zao katika maonesho bila kuwa na vibali akisema kwa atakayebianika
sheria itachukua mkondo wake.
Amesema sheria namba nne ya mwaka 2009 ambayo
ilianzisha mamlaka hiyo inawataka TANTRADE kutoa vibali kwa yeyote atakayetaka
kufanya maonesho nchini huku akisema wapo baadhi ya watu wasiyo waaminifu
hufungua maonesho bila kuomba kibali na kujiingizia kipato kinyume cha
sheria hali inayoharibu sifa ya mamlaka.
“Kuna baadhi ya wananchi hawazingatii sheria
watu wanalalamika kutapeliwa mtu anajitokeza tu anataka kufanya maonesho
wananchi wanachangia fedha mwisho tunaulizwa sisi TANTRADE jambo hili
mlilifanyaje sasa hii inaumiza wafanyabiashara niwasihi wananchi wafuatilie
kwanza kama sisi tuna taarifa hizo kabla hujatoa pesa yako hatutamuonea mtu
huruma endapo atabainika,”alisema Mwanasheria huyo.
Pia amewataka wafanyabiashara kutumia masoko
ya ndani kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora hatua itakayosaidia kuongeza wigo wa
masoko kimataifa akisema wengi wamekuwa wakilalamikia ufinyu wa masoko ya
bidhaa zao kutokana na kuzalisha kwa mazoea na kukosa elimu ya biashara.
Amesema yapo mataifa mengi Duniani ambayo
yanahitaji bidha mbalimbali kutoka Tanzania na wao kama mamlaka husika wana
wajibu wa kutafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa ajili ya wafanyabiashara
akisema wanachukua hatua kuhakikisha yanapatikana ili watanzania kupeleka
bidhaa zao.
“Kuna mahitaji makubwa ya bidhaa zetu katika
nchi za wenzetu kama matunda na nyinginezo tunawasiliana na balozi
mbalimbali na unakuta nchi husika wanasema vitu wanavyovitaka nasi
tunafahamisha umma kwa wenye uwezo wanapeleka lakini bado wajasiriamali wengi
wanazalisha bidhaa chini ya viwango,”alisema Mwanasheria huyo.
Akizungumzia fursa ya maonesho ya biashara
ambayo hufanyika kila mwaka aliwataka wafanyabiashara kuacha uwoga wa
kujitangaza na badala yake wajitokeze kushiriki kwani huwasaidia kukutana na
wafanyabiashara wakubwa hivyo kuongeza ubunifu, kupata elimu,kubadilishana
uzoefu na kujenga uhusiano wa kibiashara.
“Tuwahimize wajasiriamali na wafanyabiashara
tunaelekea katika maonesho ya biashara mwezi Juni 28 hadi 13 Julai niwaambie
huo ni mwanya mzuri unazalisha kitu fulani unakutana na mnunuzi na
wanakuwa kutoka ndani na nje ya Tanzania pia unapata changamoto utakosolewa
pale, utapewa mbinu mpya itakusaidia kuwa mzalishaji bora,”alieleza Mboya.
Mwanasheria huyo alieleza kuwa katika
utekelezaji wa majukumu yao hushirikiana na Wizara ya kilimo kujadili kwa
pamoja namna ya kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao kuleta tija
kwa kuwapatia kipato na kuongeza pato la Taifa.
“Tunafanya kazi kwa kushirikiana na malaka
zingine tunashughulika pia na kipengele cha utoaji wa elimu ya kuongeza thamani
ya bidhaa sasa tunapokutana na wizara ya kilimo inakuwa rahisi kwetu kwani wao
wako karibu zaidi na wakulima tunatamani kuona kila mkulima anafaidika na nguvu
kazi yake,”alibainisha Mboya.
Hata hivyo alieleza kwamba Mamlaka hiyo
iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo baadhi ya majukumu yao ni
utafiti wa masoko, kuwajengea uwezo na kuwaendelea wajasiriamali, kutoa huduma
za ushauri kuhusu ushindani wa kibiashara, kuendeleza bidhaa na masoko pamoja
udhibiti wa maonesho ya kimataifa ndani na nje ya nchi na kushauri
serikali katika sera na uwezeshaji.
0 Comments