📌FARIDA RAMADHANI NA PETER HAULE, WFM, DODOMA
SERIKALI imeteua Waratibu wa kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za
Fedha kwa lengo la kuimarisha
usimamizi na uendelezaji wa Sekta Fedha nchini.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Adolf Ndunguru, wakati wa ufunguzi wa awamu ya kwanza ya mafunzo
ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha.
Amesema uteuzi wa Waratibu hao ni utekelezaji wa majuku ya Waziri wa
Fedha kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 na
Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 Kifungu namba 15 pamoja na Kanuni
za Huduma Ndogo za Fedha (Majukumu ya Waziri) za mwaka 2019.
“Majukumu ya Waratibu hao yatakuwa ni kuratibu, kuhamasisha na
kutathmini biashara ya huduma ndogo za fedha katika ngazi ya Wizara, Mkoa na
Halmashauri pamoja na kusajili wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za
fedha (Microfinance Business Promoters) pamoja na kuandaa taarifa za Sekta
Ndogo ya Fedha kwa vipindi tofauti ”, alisema Bw. Ndunguru.
Amesema katika kuwawezesha Waratibu walioteuliwa kutekeleza majukumu yao
kwa umakini na ufanisi, Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa mafunzo ya awamu
mbili kwa Waratibu 212 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.
Amewataka Waratibu hao kutumia mafunzo hayo kuimarisha na kuhamasisha
Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha katika maeneo yao ya kazi kwa maendeleo na
maslahi ya wananchi hususani wenye kipato cha chini, ili waweze kuboresha
maisha yao, kuondoa umaskini, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
Awali Kamishna wa Idara ya
Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt.
Charles Mwamwaja, amesema lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa kwa Waratibu
wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa
mujibu wa Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha.
Amesema pamoja na mambo mengine Waratibu watatengeneza na kusimamia
kanzidata ya huduma ndogo za fedha, kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za
Fedha na kufuatilia na kutathmini maendeleo ya biashara hizo.
Dkt. Mwamwaja amesema Waratibu hao watasajili na kufuta usajili wa
wahamasishaji pamoja na kuandaa na kuwasilisha taarifa za huduma ndogo za fedha
kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha.
Mafunzo hayo ni muendelezo wa jitihada za Wizara ya Fedha na Mipango kwa
kushirikiana na wadau katika kutatua changamoto zilizopo katika sekta ndogo ya
fedha ili kuwezesha huduma za fedha kuwafikia wananchi wengi waishio maeneo ya
vijijini na kutimiza lengo la Serikali la kuondoa umaskini na kukuza uchumi.
0 Comments