Serikali imesema kamwe haitakuwa kikwazo kwa
wawekezaji katika kutoa vibali vya Tathmini ya Athari kwa mazingira katika
kuwezesha uwekezaji na maendeleo ya viwanda.
Kauli hii imetolewa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano ana Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu mara baada
ya kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa lengo la kukagua shughuli
za utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira
Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni
kuhakikisha kuwa inaweka mazingira Rafiki kwa wawekezaji na kutoa miongozi
katika hifadhi ya mazingira na kuliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutoa ushauri wa kitaalamu kuwezesha wawekezaji
kuzingatia Sheria.
“NEMC simamieni Sheria ya Mazingira, Viwanda
visiwe sehemu ya uchafuzi wa Mazingira ili Maendeleo ya Viwanda yaendane na
Hifadhi ya Mazingira pia NEMC msifanye kazi ya upolisi kwa kufunga Viwanda na
kutoza faini kubwa, kaeni na wenye Viwanda waelekezeni kuzingatia Sheria Waziri
Ummy alisisitiza.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemuagiza
Mkurugenzi wa Mji Kibaha kuhakikisha katika Mipango na Bajeti wanatenga fedha
kwa ajili ya ujenzi wa namna bora ya kutenganisha taka kuanzia ngazi ya kaya.
“Mkurugenzi, taka ni mali, si kila taka ziende
dampo, wekeni utaratibu4 kwenye vizimba kwa kutenganisha taka za plastiki, taka
za majumbani na taka zinazoweza kurejerezeka ili wenye viwanda vya plastiki na
vile vya kutengeneza mbolea waweze kupata malighafi Ummy alisisitiza.
Akimkaribisha katika Mkoa wa Pwani Mkuu wa
Mkoa Mhandisi Evarist Ndikilo amesema
Mkoa wake unakabiliwa na changamoto kubwa ya ukataji miti kutokana na matumizi
ya kuni na mkaa na kutoa rai kwa Wizara kuangalia uwezekano wa kuhamasisha
matumizi ya nishati mbadala ikiwemo gesi.
Pia ameshauri kuwekwa kwa utaratibu kwa wachimbaji
wa mchanga kuhakikisha kunakuwa na urejerezaji wa maeneo ya machimbo kwa
kupanda miti ili kuepuka uharibifu wa Mazingira.
Waziri Ummy amesisitiza kuwa Agenda ya
Mazingira ni suala mtambuka na kutoa rai kwa uongozi wa Mkoa wa Pwani kutumia
Sheria ndogo za Halmashauri kusimamia suala la upandaji miti kwa kuanzisha
vitalu vya miche.
Katika siku ya kwanza ya Ziara ya Waziri Ummy
Mwalimu Mkoa wa Pwani ametembelea Dampo la Mji Kibaha, Kiwanda cha Futan Mining
kinachojihusisha na uchenjuaji wa madini ya Kopa na Kiwanda cha Prance
International Ltd.
0 Comments